Zekaria 13
13
1“Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu. 2Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu. 3Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri. 4Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu, 5bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’. 6Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’”
7Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Amka, ee upanga!
Inuka umshambulie mchungaji wangu;
naam, mchungaji anayenitumikia.
Mpige mchungaji na kondoo watawanyike.
Nitaunyosha mkono wangu,
kuwashambulia watu wadhaifu.
8Theluthi mbili za watu katika nchi zitaangamizwa;
ni theluthi moja tu itakayosalimika.
9Theluthi hiyo moja itakayosalia,
nitaijaribu na kuitakasa,
kama mtu asafishavyo fedha,
naam, kama ijaribiwavyo dhahabu.
Hapo wao wataniomba mimi,
nami nitawajibu.
Nitasema, ‘Hawa ni watu wangu’,
nao watasema, ‘Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu.’”
Currently Selected:
Zekaria 13: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.