Waroma 3
3
1Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? 2Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. 3Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? 4Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Kila usemapo,
maneno yako ni ya kweli;
na katika hukumu,
wewe hushinda.”
5Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). 6Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu?
7Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” 8Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili!
Hakuna mtu yeyote aliye mwadilifu
9Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. 10#Taz Zab 14:1-3; 53:1-3 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu!
11Hakuna mtu anayeelewa,
wala anayemtafuta Mungu.
12Wote wamepotoka
wote wamekosa;
hakuna atendaye mema,
hakuna hata mmoja.
13 # Taz Zab 5:9; 140:3 Makoo yao ni kama kaburi wazi,
ndimi zao zimejaa udanganyifu,
midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka.
14 # Taz Zab 10:7 Vinywa vyao vimejaa laana chungu.
15Miguu yao iko mbioni kumwaga damu,
16popote waendapo husababisha maafa na mateso;
17njia ya amani hawaijui.
18 # Taz Zab 36:1 Hawajali kabisa kumcha Mungu.”
19Tunajua kwamba sheria huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. 20#Taz Zab 143:2 Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi.
Kukubaliwa na Mungu kwa imani
21Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. 22Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. 23Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. 24Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. 25Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; 26sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.
27Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini. 28Maana Mungu humkubali mtu kuwa mwadilifu kwa imani, wala si kwa kutimiza matakwa ya sheria. 29Au je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa mataifa mengine? Naam, wa watu wa mataifa mengine pia. 30Mungu ni mmoja, naye atawafanya Wayahudi kuwa waadilifu kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao. 31Je, tunaitumia imani kuibatilisha sheria? Hata kidogo; bali tunaipa sheria thamani yake kamili.
Currently Selected:
Waroma 3: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.