Yobu 12
12
Jibu la Yobu
1Ndipo Yobu akajibu:
2“Sawa! Nyinyi ni watu wa hekima.
Hekima itakufa wakati ule mtakapokufa.
3Mimi nami ni mwelewa kama nyinyi.
Mimi si mtu duni kuliko nyinyi.
Yote mliyosema kila mtu anajua.
4Nimekuwa kichekesho kwa rafiki zangu:
Mimi niliyemwomba Mungu na akanijibu;
mimi niliye mwadilifu na bila lawama,
nimekuwa kichekesho kwa watu.
5Mtu anayestarehe hudharau msiba;
kwake, msiba huwajia wale wanaoteleza.
6Makao ya wanyanganyi yana amani;
wenye kumchokoza Mungu wako salama,
nguvu yao ni mungu wao.
7Lakini waulize wanyama nao watakufunza;
waulize ndege nao watakuambia.
8Au iulize mimea nayo itakufundisha;
sema na samaki nao watakuarifu.
9Nani kati ya viumbe hivyo,
asiyejua kwamba Mwenyezi-Mungu ametenda hayo?
10Uhai wa kila kiumbe hai umo mikononi mwake;
kadhalika na pumzi ya uhai wa binadamu.
11Je, sikio haliyapimi maneno
kama ulimi uonjavyo chakula?
12Hekima iko kwa watu wazee,
maarifa kwao walioishi muda mrefu.
13Lakini hekima na uwezo ni vyake Mungu,
yeye ana maarifa na ujuzi.
14Akibomoa, hakuna awezaye kujenga upya;
akimfunga mtu, hakuna awezaye kumfungua.
15Akizuia mvua, twapata ukame;
akiifungulia, nchi hupata mafuriko.
16Yeye ana nguvu na hekima;
wanaodanganywa na wanaodanganya ni wake.
17Huwaacha washauri waende zao uchi,
huwafanya waamuzi kuwa wapumbavu.
18Huwavua wafalme vilemba vyao;
na kuwafunga viunoni kamba za wafungwa;
19Huwaacha makuhani waende uchi;
na kuwaangusha wenye nguvu.
20Huwanyanganya washauri kipawa chao cha kuongea,
huwapokonya wazee hekima yao.
21Huwamwagia wakuu aibu,
huwaondolea wenye uwezo nguvu zao.
22Huvifunua vilindi vya giza,
na kuleta mwangani yaliyokuwa gizani.
23Huyakuza mataifa kisha huyaangamiza,
huyafanya yapanuke kisha huyatawanya.
24Huwaondolea viongozi wa watu ujuzi wao,
huwafanya watangetange nyikani kusiko na njia,
25wakapapasapapasa gizani kusiko na mwanga;
na kuwafanya wapepesuke kama walevi.
Currently Selected:
Yobu 12: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.