Isaya 50
50
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Kama nimempa talaka mama yako Yerusalemu,
hati ya talaka iko wapi?
Au kama niliwauza utumwani,
yuko wapi basi, huyo niliyemwuzia?
Kumbukeni mliuzwa utumwani kwa maovu yenu,
mama yenu alifukuzwa kwa makosa yenu.
2“Nilipokuja kwa nini sikukuta mtu?
Nilipoita mbona hamkuitikia?
Je, mkono wangu ni mfupi nisiweze kuwaokoeni?
Je, sina nguvu ya kuwakomboa?
Tazama! Kwa kuikemea kidogo bahari hukauka,
na mito nikaifanya kuwa jangwa,
samaki wake wakafa na kunuka kwa kukosa maji.
3Mimi hulivika anga giza,
na kulivalisha vazi la kuomboleza.”
Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu
4Bwana Mungu amenipa ufasaha wa lugha,
niwatie moyo wale waliochoka.
Kila asubuhi hunipa hamu
ya kusikiliza anayotaka kunifunza.
5Bwana Mungu amenifanya msikivu,
nami sikuwa mkaidi
wala kugeuka mbali naye.
6 #50:6 Taz Mat 26:67; Marko 14:65 Mgongo wangu niliwaachia walionipiga,
mashavu yangu waliozingoa ndevu zangu;
walioniaibisha na kunitemea mate,
sikujificha mbali nao.
7Bwana Mungu hunisaidia,
kwa hiyo siwezi kufadhaika.
Uso wangu nimeukaza kama jiwe;
najua kwamba sitaaibishwa.
8 #50:8-9 Taz Rom 8:33-34 Mtetezi wangu yuko karibu.
Ni nani atakayepingana nami?
Na aje tusimame mahakamani.
Adui yangu ni nani?
Na ajitokeze mbele basi.
9Tazama Bwana Mungu hunisaidia.
Ni nani awezaye kusema nina hatia?
Maadui zangu wote watachakaa kama vazi,
nondo watawatafuna.
10Nani kati yenu amchaye Mwenyezi-Mungu?
Nani anayetii maneno ya mtumishi wake?
Kama yupo atembeaye gizani bila taa,
amtumainie Mwenyezi-Mungu,
na kumtegemea Mungu wake.
11Lakini nyinyi mnaowasha moto,
na kujifanyia silaha za mienge,
tembeeni kwa mwanga wa moto huo,
miali ya moto mliowasha nyinyi wenyewe.
Mtakachopata kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ni hiki:
Nyinyi mtalala chini na mateso makali.
Currently Selected:
Isaya 50: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.