Isaya 2
2
Amani ya kudumu
(Mika 4:1-3)
1Neno alilopewa Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na Yerusalemu.
2Siku zijazo mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu
utaimarishwa kupita milima yote,
utainuliwa juu ya vilima vyote.
Mataifa yote yatamiminika huko,
3watu wengi wataujia na kusema,
“Njoni tupande mlima wa Mwenyezi-Mungu,
twende nyumbani kwa Mungu wa Yakobo,
apate kutufundisha njia zake,
nasi tuishi kadiri ya mwongozo wake.
Maana sheria itakuja kutoka Siyoni;
neno la Mwenyezi-Mungu kutoka Yerusalemu.”
4 #2:4 Taz Yoe 3:10 Mungu atasuluhisha mizozo ya mataifa
atakata mashauri ya watu wengi.
Watu watafua panga za vita kuwa majembe
na mikuki yao kuwa miundu ya kupogolea.
Taifa halitapigana na taifa lingine
wala hayatafanya tena mazoezi ya vita.
5Sasa, enyi wazawa wa Yakobo, njoni,
tutembee katika mwanga wa Mwenyezi-Mungu.
Kiburi kitaondolewa
6Sasa, ee Mungu, umewatupa watu wako, wazawa wa Yakobo.
Maana kweli wachawi wa mashariki wamejaa kati yao,
wapo na wapiga ramli kama kwa Wafilisti.
Wanashirikiana na watu wageni.
7Nchi yao imejaa fedha na dhahabu,
hazina yao ni kubwa kupindukia.
Nchi yao imejaa farasi,
magari yao ya kukokotwa hayana idadi.
8Nchi yao imejaa vinyago vya miungu,
huabudu kazi ya mikono yao,
vitu walivyotengeneza wao wenyewe.
9Kwa hiyo, kila mtu ataaibishwa na kufedheheshwa.
Usiwasamehe hata kidogo, ee Mungu!
10 #2:10 Taz Ufu 6:15; 2Thes 1:9 Ingieni katika mwamba,
mkajifiche mavumbini,
kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu,
mbali na utukufu wa enzi yake.
11Siku yaja ambapo kiburi cha watu kitashushwa,
majivuno ya kila mtu yatavunjwa;
na Mwenyezi-Mungu peke yake atatukuzwa siku hiyo.
12Naam, yaja siku ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi
dhidi ya wenye kiburi na majivuno,
dhidi ya wote wanaojikweza;
13dhidi ya mierezi yote ya Lebanoni,
ambayo ni mirefu na mizuri,
dhidi ya mialoni yote nchini Bashani;
14dhidi ya milima yote mirefu,
dhidi ya vilima vyote vya juu;
15dhidi ya minara yote mirefu,
dhidi ya kuta zote za ngome;
16dhidi ya meli zote za Tarshishi,
na dhidi ya meli zote nzuri.
17Kiburi chote cha watu kitakomeshwa,
majivuno ya kila mtu yatavunjwa.
Na Mwenyezi-Mungu peke yake atatukuzwa siku hiyo.
18Vinyago vyote vya miungu vitatoweka kabisa.
19Ingieni katika mapango miambani,
katika mashimo ardhini,
kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu,
mbali na utukufu wa enzi yake,
atakapokuja kuitia hofu dunia.
20Siku hiyo, watu watawatupia panya na popo
vinyago vyao vya fedha na dhahabu
walivyojitengenezea ili kuviabudu.
21Nao wataingia katika mapango miambani
na kwenye nyufa za miamba,
kuiepa hasira ya Mwenyezi-Mungu,
mbali na utukufu wa enzi yake,
atakapokuja kuitia hofu dunia.
22Usimwamini binadamu,
uhai wake haudumu kama pumzi.
Yeye anafaa kitu gani?
Currently Selected:
Isaya 2: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.