Kumbukumbu la Sheria 33
33
Mose anayabariki makabila ya Israeli
1Hii ndiyo baraka ambayo Mose, mtu wa Mungu aliwatakia Waisraeli kabla ya kufariki kwake. Alisema:
2Mwenyezi-Mungu alikuja kutoka mlima Sinai,
alitutokea kutoka mlima Seiri;
aliiangaza kutoka mlima Parani.
Alitokea kati ya maelfu ya malaika,
na moto uwakao katika mkono wake wa kulia.
3Mwenyezi-Mungu aliwapenda watu wake;
na huwalinda watakatifu wake wote.
Hivyo, malaika wake walifuata nyayo zake,
na kupata maagizo kutoka kwake.
4Mose alituamuru tutii sheria;
kitu cha thamani kuu cha taifa letu.
5Mwenyezi-Mungu akawa mfalme wa Israeli,
wakati viongozi wao walipokutana,
na makabila yote yalipokusanyika.
6Mose alisema juu ya kabila la Reubeni:
“Reubeni aishi wala asife,
na watu wake wasiwe wachache.”
7Juu ya kabila la Yuda alisema:
“Ee Mwenyezi-Mungu usikilize kilio cha kabila la Yuda;
umrudishe tena kwa watu wale wengine.
Upigane kwa mikono yako kwa ajili yake,
ulisaidie kabila la Yuda dhidi ya adui zake.”
8Juu ya kabila la Lawi, alisema:
“Ee Mwenyezi-Mungu ulipatie Lawi kauli yako ya Urimu,
kauli yako ya thumimu#33:8 kauli yako … kauli yako: Kiebrania: Urimu, Thumimu. Taz Kut 28:30 kwa hao waaminifu wako,
ambao uliwajaribu huko Masa.
9Ulishindana nao kwenye maji ya Meriba.
Walawi walioamua kuwaacha wazee wao,
wakawasahau jamaa zao,
wasiwatambue hata watoto wao
maana walizingatia amri zako,
na kushika agano lako.
10Na wawafundishe wazawa wa Yakobo maagizo yako;
wawafundishe watu wa Israeli sheria yako.
Walawi na wafukize ubani mbele yako,
sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni pako.
11Ee Mwenyezi-Mungu, uzibariki nguvu zao,
uzikubali kazi za mikono yao;
uzivunjilie mbali nguvu za maadui zao,
nguvu za wanaowachukia hata wasiinuke tena.”
12Juu ya kabila la Benyamini alisema:
“Hili ni kabila alipendalo Mwenyezi-Mungu,
nalo hukaa salama karibu naye.
Yeye hulilinda mchana kutwa,
na kukaa kati ya milima#33:12 milima: Neno kwa neno: Mabega. yake.”
13Juu ya kabila la Yosefu alisema:
“Mwenyezi-Mungu na aibariki nchi yake,
kwa baraka nzuri kabisa kutoka juu,
14ibarikiwe kwa matunda bora yalioiva kwa jua,
kwa matunda ya kila mwezi;
15kwa mazao bora ya milima ya kale,
na mazao tele ya milima ya kale,
16Nchi yake ijae yote yaliyo mema,
ibarikiwe kwa wema wa Mwenyezi-Mungu,
ambaye alitokea katika kichaka.
Baraka hizi ziwashukie watu wa kabila la Yosefu,
aliyekuwa mkuu miongoni mwa ndugu zake.
17Fahari yake ni fahari ya fahali wa kwanza,
pembe zake ni za nyati dume.
Atazitumia kuyasukuma mataifa;
yote atayasukuma mpaka miisho ya dunia.
Efraimu atakuwa na pembe hizo 10,000
na Manase kwa maelfu.”
18Juu ya kabila la Zebuluni na kabila la Isakari, alisema,
“Zebuluni, furahi katika safari zako;
nawe Isakari, furahi katika mahema yako.
19Watawaalika wageni kwenye milima yao,
na huko watu watatoa sadaka zinazotakiwa.
Maana wao watapata utajiri wao kutoka baharini
na hazina zao katika mchanga wa pwani.”
20Juu ya kabila la Gadi, alisema:
“Atukuzwe Mungu ampatiaye Gadi sehemu kubwa.
Gadi hunyemelea kama simba
akwanyue mkono na utosi wa kichwa.
21Alijichagulia eneo zuri kuliko yote,
mahali ilipotengwa sehemu ya kiongozi.
Aliwaongoza watu na kumtii Mwenyezi-Mungu,
alitekeleza mpango wa Mungu kwa Israeli.”
22Juu ya kabila la Dani alisema hivi:
“Dani ni mwanasimba
arukaye kutoka Bashani.”
23Juu ya kabila la Naftali alisema:
“Ee Naftali fadhili,
uliyejaa baraka za Mwenyezi-Mungu,
nchi yako ni kusini kwenye ziwa Kinerethi.”
24Juu ya kabila la Asheri alisema:
“Asheri abarikiwe kuliko watoto wote wa Yakobo,
na upendelewe na ndugu zako wote;
na achovye mguu wake katika mafuta.
25Miji yako ni ngome za chuma na shaba.
Usalama wako utadumu maisha yako yote!”
26Mose akamalizia kwa kusema,
“Ee Israeli, hakuna aliye kama Mungu wako,
yeye hupita mbinguni kuja kukusaidia,
hupita juu angani katika utukufu wake.
27Mungu wa milele ndiye kimbilio lenu;
nguvu yake yaonekana duniani.
Aliwafukuza maadui mbele yenu;
aliwaamuru: ‘Waangamizeni.’
28Kwa hiyo, watu wa Israeli wakakaa salama,
wazawa wa Yakobo peke yao,
katika nchi iliyojaa nafaka na divai,
nchi ambayo anga lake hudondosha umande.
29Heri yenu nyinyi Waisraeli.
Nani aliye kama nyinyi, watu mliookolewa na Mwenyezi-Mungu,
ambaye ndiye ngao ya msaada wenu,
na upanga unaowaletea ushindi!
Adui zenu watakuja wananyenyekea mbele yenu,
nanyi mtawakanyaga chini.”
Currently Selected:
Kumbukumbu la Sheria 33: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.