Amosi 1
1
Nabii Amosi
1Maneno ya Amosi, mmojawapo wa wachungaji wa mji wa Tekoa. Mungu alimfunulia Amosi mambo haya yote kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya lile tetemeko la ardhi, wakati Uzia alipokuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, alipokuwa mfalme wa Israeli. 2Amosi alisema hivi:
Mwenyezi-Mungu ananguruma kutoka mlima Siyoni,
anavumisha sauti yake kutoka Yerusalemu,
hata malisho ya wachungaji yanakauka,
nyasi mlimani Karmeli zinanyauka.
Hukumu ya Mungu kwa mataifa jirani ya Israeli
Damasko
3Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Damasko wametenda dhambi tena na tena;
kwa hiyo, sitaacha kuwaadhibu;
waliwatendea watu wa Gileadi ukatili mbaya.
4Basi, nitaishushia moto ikulu ya mfalme Hazaeli,
nao utaziteketeza kabisa ngome za mfalme Ben-hadadi.
5Nitayavunjavunja malango ya mji wa Damasko,
na kuwang'oa wakazi wa bonde la Aweni,
pamoja na mtawala wa Beth-edeni.
Watu wa Aramu watapelekwa uhamishoni Kiri.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Filistia
6Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Gaza wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Walichukua mateka watu kabila zima,
wakawauza wawe watumwa kwa Waedomu.
7Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Gaza,
nao utaziteketeza kabisa ngome zake.
8Nitawang'oa wakazi wa mji wa Ashdodi,
pamoja na mtawala wa Ashkeloni.
Nitanyosha mkono dhidi ya Ekroni,
nao Wafilisti wote waliosalia wataangamia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Tiro
9Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Tiro wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Walichukua mateka kabila zima hadi Edomu,
wakaukiuka mkataba wa urafiki waliokuwa wamefanya.
10Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Tiro,
na kuziteketeza kabisa ngome zake.”
Edomu
11Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Edomu wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Waliwawinda ndugu zao#1:11 ndugu zao: Waisraeli walikuwa wazawa wa Yakobo, nduguye Esau, wazee wao Waedomu. Waisraeli kwa mapanga,
wakaitupilia mbali huruma yao yote ya kindugu.
Hasira yao haikuwa na kikomo,
waliiacha iwake daima.
12Basi, nitaushushia moto mji wa Temani,
na kuziteketeza kabisa ngome za Bosra.”
Amoni
13Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu wa Amoni wametenda dhambi tena na tena,
kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu.
Katika vita vyao vya kupora nchi zaidi,
waliwatumbua wanawake waja wazito nchini Gileadi.
14Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Raba,
na kuziteketeza kabisa ngome zake.
Siku hiyo ya vita patakuwa na makelele mengi,
nayo mapambano yatakuwa makali kama tufani.
15Mfalme wao na maofisa wake,
wote watakwenda kukaa uhamishoni.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Currently Selected:
Amosi 1: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.