YouVersion Logo
Search Icon

Methali 25

25
Methali zaidi za Solomoni
1Hizi nazo ni methali nyingine za mfalme Solomoni walizonakili watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda.
2Mungu hutukuzwa kwa kuficha mambo,
lakini mfalme hutukuzwa kwa yale anayoeleza.
3Kama zilivyo mbali mbingu na kirefu kina cha ardhi
ndivyo zisivyochunguzika akili za mfalme.
4Toa takataka katika fedha,
na mhunzi atakutengenezea chombo kizuri.
5Waondoe waovu mbele ya mfalme,
na utawala wake utaimarika katika haki.
6Usijipendekeze kwa mfalme,
wala usijifanye mtu mkubwa,
7maana ni heri kuambiwa, “Njoo huku mbele”,
kuliko kuporomoshwa mbele ya mkuu.
Mambo uliyoyaona kwa macho yako,
8usiharakishe kuyapeleka mahakamani;
maana utafanya nini hapo baadaye,
shahidi mwingine akibatilisha hayo usemayo?
9Suluhisha ugomvi na mwenzako peke yake,
na kila mmoja wenu asitoe siri ya mwenzake;
10watu wasije wakajua kuna siri,
ukajiharibia jina lako daima.
11Neno lisemwalo wakati unaofaa,
ni kama nakshi za dhahabu juu ya madini ya fedha.
12Onyo la mwenye hekima kwa mtu msikivu,
ni bora kuliko pete au vito vya dhahabu safi.
13Mjumbe mwaminifu humfurahisha yule aliyemtuma,
kama maji baridi wakati wa joto la mavuno.
14Kama vile mawingu na upepo bila mvua,
ndivyo alivyo mtu anayejigamba kutoa zawadi asiitoe.
15Kwa uvumilivu mtawala huweza kushawishika;
ulimi laini huvunja mifupa.
16Upatapo asali kula kiasi cha kukutosha,
usije ukaikinai na kuitapika.
17Usimtembelee jirani yako mara kwa mara,
usije ukamchosha naye akakuchukia.
18Mtu atoaye ushahidi wa uongo dhidi ya mwenziwe,
ni hatari kama rungu, upanga au mshale mkali.
19Kumtegemea mtu asiyeaminika wakati wa taabu,
ni kama jino bovu au mguu ulioteguka.
20Kumwimbia mtu mwenye huzuni,
ni kama kuvua nguo wakati wa baridi,
au kutia siki katika kidonda.
21Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula;
akiwa na kiu, mpe maji ya kunywa.
22Hivyo utafanya apate aibu kali,
kama makaa ya moto kichwani pake,
naye Mwenyezi-Mungu atakutuza.
23Upepo wa kusi huleta mvua,
hali kadhalika masengenyo huleta chuki.
24Afadhali kuishi pembeni juu ya paa,
kuliko kuishi nyumbani pamoja na mwanamke mgomvi.
25Kama vile maji baridi kwa mwenye kiu,
ndivyo habari njema kutoka mbali.
26Mwadilifu akubaliye kufuata mambo ya mwovu,
ni chemchemi iliyochafuliwa au kisima kilichotibuliwa.
27Si vizuri kula asali nyingi mno;
kadhalika haifai kujipendekeza mno.#25:27 kadhalika … mno: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
28Mtu asiyeweza kuzuia hasira yake,
ni kama mji usio na ulinzi unaposhambuliwa.

Currently Selected:

Methali 25: BHND

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in