2 Wamakabayo 4
4
Simoni amshtaki Onia
1Lakini Simoni (aliyetajwa huko nyuma kwamba alimwarifu Apolonio kuhusu hiyo fedha na hivi akasababisha matatizo kwa taifa) alimsingizia Onia, akidai eti yeye ndiye aliyemchochea Heliodoro na kusababisha shida zilizofuata. 2Alithubutu kumshtaki Onia eti alifanya hila dhidi ya serikali - Onia ambaye si tu alikuwa mkarimu kwa Yerusalemu na kulilinda hekalu, bali pia alikuwa macho kuangalia kwamba sheria zetu zote zinashikwa! 3Chuki ya Simoni ilizidi kuongezeka hata baadhi ya maajenti wake wakaua watu kadha. 4Onia alitambua kwamba hali ilikuwa ya hatari, na kwamba Apolonio mwana wa Menestheo, mkuu wa Siria Kuu na Foinike alikuwa anamtia moyo Simoni katika kila ovu alilofanya. 5Basi, akamwendea mfalme, si kwa nia ya kuwashtaki wananchi wenzake, ila kwa manufaa ya Wayahudi wote, katika maisha yao ya nyumbani na ya hadharani. 6Alijua kwamba bila ya ushirikiano wa mfalme amani isingepatikana, na Simoni angeendelea na upumbavu wake.
Yasoni aingiza utamaduni wa Kigiriki
7Baadaye, mfalme Seleuko alipofariki dunia na Antioko (aliyejulikana kama Epifane) kushika wadhifa huo, Yasoni nduguye Onia, akajipatia ukuhani mkuu kwa njia haramu. 8Alikwenda kumwona mfalme, akampa fedha kilo 12,000, akiahidi kuongeza kilo 2,700 baadaye. 9Aidha, Yasoni alimpa mfalme fedha kilo 5,000 ili kupata idhini ya kuanzisha kiwanja cha michezo kwa ajili ya mazoezi ya vijana, na idhini ya kuwaandikisha watu wa Yerusalemu uraia wa Antiokia.
10Mfalme aliidhinisha hayo. Na mara tu Yasoni alipojichukulia wadhifa wa kuhani mkuu, aliwafanya watu wa Yerusalemu waache utamaduni wao na kuanza kuishi kama Wagiriki. 11Alianza kwa kufutilia mbali upendeleo wa kifalme ambao Wayahudi walipatiwa kwa njia ya Yohane, baba yake Eupolemo, ambaye baadaye alikwenda kufanya mkataba wa urafiki na ushirika na Waroma. Kisha, Yasoni akafutilia mbali mila na desturi zetu za Kiyahudi, akaingiza utamaduni mpya uliopingana na sheria yetu. 12Kwa ari na msisimko mkubwa alijenga uwanja wa michezo karibu na mlima wa hekalu, akawashawishi vijana wetu wazuri waige mila na desturi za Kigiriki. 13Kutokana na uovu usio na kifani wa Yasoni, huyo kuhani mkuu haramu na asiyemcha Mungu, hali ya kupenda sana kuishi kama Wagiriki na ya kuiga desturi za kigeni iliongezeka mno, 14hata makuhani hawakuwa na mvuto tena juu ya huduma yao madhabahuni. Walipuuza mahali patakatifu na kuacha kutoa tambiko; na mara waliposikia kipenga cha kuanza michezo, walikwenda mbio uwanjani mwa mieleka kushiriki michezo iliyokatazwa na sheria yetu. 15Hawakujali chochote kile kilichokuwa kimethaminiwa na wazee wao, ila walithamini mambo ya Kigiriki tu. 16Kwa hiyo wakapatwa na misiba mikubwa hata watu haohao ambao mila na desturi zao walizisifia na kujaribu kuiga, ndio hao waliogeuka kuwa maadui zao, na kuwakandamiza. 17Naam, kuipuuza sheria ya Mungu si jambo la mchezo, kama utakavyoona huko mbele.
Yerusalemu yaathiriwa na Siria
18Siku moja mfalme alipohudhuria michezo ya riadha ambayo ilikuwa ikifanyika mjini Tirza kila mwaka wa tano,#4:18 tano: Au nne. 19huyo mshenzi Yasoni akawatuma watu huko Tirza kutoka Yerusalemu, watu ambao walikuwa raia wa Antiokia, kupeleka fedha 10,000 kwa ajili ya kugharimia tambiko kwa mungu Herkule. Lakini hata watu hao hawakuona inafaa kutumia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya tambiko, na 20hivi, fedha hiyo ambayo kwanza ilinuiwa itolewe tambiko kwa Herkule, ikatumika kwa ajili ya kutengeneza meli za vita.
21Apolonio, mwana wa Menestheo, alipotumwa Misri kuhudhuria sherehe ya kutawazwa kwake mfalme Filometori, Antioko alipata habari kwamba Filometori alikuwa anapingana na siasa yake. Basi, Antioko akawa na wasiwasi juu ya usalama wa utawala wake, hivi akaenda Yopa, na halafu Yerusalemu. 22Huko alipokewa kwa heshima kubwa na Yasoni na watu wa mjini ambao walitoka nje kumlaki na kelele za shangwe, huku wamechukua mienge ya moto. Kutoka Yerusalemu Antioko alikwenda na jeshi lake Foinike.
Menelao awa kuhani mkuu
23Miaka mitatu baadaye, Yasoni alimtuma Menelao, ndugu ya Simoni aliyetajwa hapo awali, kumpelekea fedha mfalme na kukamilisha idadi ya mambo kadha muhimu. 24Lakini aliposimama mbele ya mfalme, Menelao akajipendekeza kwa kuonesha mamlaka yake, na akatoa fedha kilo 10,000 zaidi kuliko alivyotoa Yasoni ili ateuliwe yeye kuwa kuhani mkuu. 25Hivi Menelao akarejea Yerusalemu na hati za mfalme za kumthibitisha kuwa kuhani mkuu. Lakini hakuwa na sifa za ukuhani mkuu, bali alikuwa mdhalimu mwenye hasira kali, na mkali kama mnyama. 26Hivyo Yasoni, aliyekuwa amemnyang'anya ukuhani mkuu nduguye kwa hila, sasa naye akawa amenyang'anywa, alilazimika kukimbilia nchi ya Amoni. 27Menelao aliendelea kuwa kuhani mkuu, lakini kamwe hakulipa hata senti moja ya fedha aliyomwahidia mfalme. 28Wakati Sostrato, kapteni wa ngome ya Yerusalemu, alipoendelea kudai fedha hiyo, kwa vile ulikuwa wajibu wake kukusanya fedha hiyo, hao wawili waliitwa mbele ya mfalme kuhusu suala hilo. 29Menelao akampa nduguye Lisimako wadhifa wa naibu kuhani mkuu; ambapo Sostrato akampa wadhifa huo Krate, kamanda wa jeshi la Kupro.
Kuuawa kwa Onia
30Wakati huo huo yakatokea maasi katika miji ya Tarso na Malo kwa sababu mfalme alikuwa amempa miji hiyo Antioki, suria wake. 31Kwa hiyo akaondoka kwa haraka kwenda kurekebisha mambo Kilikia, akimwachia mamlaka Androniko, mmoja wa maofisa wake wakuu. 32Menelao akaitumia vizuri fursa hiyo. Akampa Androniko baadhi ya vitu vya dhahabu alivyokuwa ameviondoa kutoka hekalu la Yerusalemu; alikuwa amekwisha iuzia miji ya Tirza na mingine ya jirani baadhi ya vifaa hivyo. 33Onia alipopata habari kamili juu ya hayo akakimbilia kujisalimisha kwenye hekalu moja huko Dafne, karibu na mji wa Antiokia. Huko akamlaumu na kumwathiri Menelao hadharani. 34Ndipo Menelao akambembeleza Androniko faraghani amuulie mbali Onia. Basi, Androniko akamwendea Onia na kumdanganya kwa maneno ya kirafiki na ahadi za kumhakikishia usalama. Ingawa Onia alitia shaka, Androniko hatimaye alifaulu kumwondoa mle hekaluni kwenye usalama, akamuua mara bila kujali haki.
Androniko aadhibiwa
35Wayahudi na watu wa mataifa mengine walikasirishwa sana na mauaji hayo ya kidhalimu. 36Hivi mfalme aliporejea kutoka nchini Kilikia, Wayahudi wa Antiokia wakamwendea na kupinga mauaji hayo ya kijinga; hata Wagiriki wakaonesha chuki yao dhidi ya uovu huo. 37Mfalme Antioko alisikitika na kuhuzunika hata machozi yakamtoka, hasa alipokumbuka Onia alivyokuwa na busara, na alivyokuwa na kiasi na mtaratibu. 38Akiwa amewaka hasira, Antioko alirarulia mbali vazi la urujuani la Androniko, halafu akamtembeza kuzunguka mji mpaka mahali alipomwulia Onia. Na hapo akamuua naye. Hivyo ndivyo Bwana alivyomwadhibu Androniko kama alivyostahili.
Kuuawa kwa Lisimako
39Wakati huo huo, Lisimako akisaidiwa na nduguye, Menelao, alikuwa amefanya vitendo vingi mjini vya kufuru na vifaa vingi vya dhahabu kuibiwa hekaluni. Habari hiyo ilipoenea, watu, makundi kwa makundi, wakaanza kukusanyika kumpinga Lisimako. 40Mwishowe haikuwezekana kuyatawala makundi hayo yaliyozidi kuchachamaa. Basi, Lisimako akapeleka kikosi cha watu 3,000 wenye silaha, kuyashambulia hayo makundi, kikosi hicho kiliongozwa na Aurano, aliyekuwa mzee na mfidhuli kupindukia. 41Wayahudi waliokuwa katika ua wa hekalu walipoona karibu kushambuliwa, wakaokota mawe, kuni na hata majivu kutoka madhabahuni, wakawatupia akina Lisimako katika ghasia hiyo. 42Waliwaua wachache miongoni mwa watu wa Lisimako, wakawajeruhi wengi wao, na wote waliobaki wakakimbia kusalimisha maisha yao. Lisimako mwenyewe, lile jizi la vitu vya hekalu, aliuawa karibu na hazina ya hekalu.
Menelao ashtakiwa
43Kwa sababu ya tukio hilo, Menelao alishtakiwa. 44Mfalme alipofika mjini Tirza, wakuu wa Wayahudi wa Yerusalemu waliwatuma watu watatu kwake kutoa mashtaka dhidi ya Menelao. 45Menelao alipoona kesi inamlemea, akampa hongo kubwa Tolemai, mwana wa Dorimene, ili amlainishe mfalme ampendelee. 46Tolemai akamsihi mfalme atoke nje pamoja naye, wakapunge upepo. Huko akamshawishi abadilishe uamuzi wake 47na kutangaza kwamba Menelao hana hatia yoyote. Hivi, Menelao akaachiliwa huru, ingawa alikuwa amesababisha matatizo yale yote; lakini wale watu watatu, ambao hata kama wangalijitetea mbele ya wafidhuli wangetangazwa hawana hatia, walihukumiwa adhabu ya kifo. 48Wale watu watatu walikuwa wameongea kutetea Yerusalemu, watu wake,#4:48 watu wake: Hati nyingine zina: Vijiji vya jirani. na vyombo vitakatifu vilivyokuwa vimeibwa kutoka hekaluni; lakini waliadhibiwa upesi na bila ya haki. 49Baadhi ya watu wa Tirza, hata hivyo, walionesha kuchukizwa kwao na uovu huo, wakadhihirisha heshima yao kwa kuwazika marehemu vizuri sana. 50Menelao aliendelea na wadhifa wake kwa sababu ya ulafi wa wale waliokuwa madarakani. Kila siku alikuwa mwovu zaidi, akawa adui mbaya kabisa wa raia wenzake.
Currently Selected:
2 Wamakabayo 4: BHND
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Learn More About Biblia Habari Njema