2 Wakorintho 13
13
Maonyo ya mwisho na salamu
1Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. “Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu,” yasema Maandiko. 2Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: Wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, sitakuwa na huruma. 3Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu. 4Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu.
5Jichunguzeni nyinyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni nyinyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi nyinyi mmeshindwa. 6Lakini natumaini kwamba nyinyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa. 7Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa. 8Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli. 9Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini nyinyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu. 10Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa. 11Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.
12Salimianeni kwa ishara ya upendo. 13Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni.
14Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.
Currently Selected:
2 Wakorintho 13: BHND
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Learn More About Biblia Habari Njema