YouVersion Logo
Search Icon

Luka 6

6
Swali kuhusu sabato
1 # Mt 12:1-8; Mk 2:23-28 Ikawa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusapukusa mikononi mwao.#Kum 23:25 2#Yn 5:10 Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? 3#1 Sam 21:1-6 Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? 4#Law 24:9 Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao. 5Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
Mtu mwenye mkono uliopooza
6 # Mt 12:9-14; Mk 3:1-6 Ikawa siku ya sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kulia umepooza. 7#Lk 14:1 Na Waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kama ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. 8Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. 9Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? 10Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. 11Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.
Yesu achagua wanafunzi kumi na wawili
12 # Mk 3:13-19 Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu. 13#Mt 10:2-4; Yn 6:70; Mdo 1:13 Na kulipokucha aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita mitume; 14Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartholomayo, 15na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, 16na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskarioti, ndiye aliyekuwa msaliti.
Yesu afundisha na kuponya
17 # Mt 4:23—5:1; Mk 3:7-12 Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Yudea wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao; 18na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa. 19Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.
Baraka na masikitiko
20 # Mt 5:3,4,6,11,12 Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. 21#Ufu 7:16,17; Zab 126:5,6; Isa 61:3 Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka. 22#1 Pet 4:14; Yn 15:19; 16:2 Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. 23#2 Nya 36:16; Mdo 7:52 Furahieni siku ile na kurukaruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo. 24#Yak 5:1 Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata. 25#Isa 5:22 Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. 26#Yak 4:4; Mik 2:11 Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.
Upendo kwa adui
27 # Mt 5:39-48 Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, 28wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. 29Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. 30Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. 31#Mt 7:12 Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. 32Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. 33Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. 34#Law 25:35,36 Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. 35Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. 36Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.
Kuwahukumu wengine
37 # Mt 7:1-29 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; sameheni, nanyi mtasamehewa.#Mt 6:14 38#Mk 4:24 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.
39 # Mt 15:14; 23:16,24 Akawaambia mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? 40#Mt 10:24-25; Yn 13:16; 15:20 Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. 41Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? 42Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.
Mti na matunda yake
43Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; 44#Mt 12:33 kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. 45#Mt 12:34,35 Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.
Misingi miwili
46 # Mal 1:6; Mt 7:21 Na kwa nini mnaniita, Bwana, Bwana, lakini hamyatendi nisemayo? 47Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonesha mfano wake. 48Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliipiga nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. 49Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaipiga kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba ile yakawa makubwa.

Currently Selected:

Luka 6: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in