YouVersion Logo
Search Icon

Ayubu 28

28
Hekima inapopatikana
1Hakika kuna shimo wachimbako fedha,
Na mahali wapatapo dhahabu waisafishayo.
2Chuma hufukuliwa katika ardhi,
Na shaba huyeyushwa katika mawe.
3 # Mit 2:4; Mhu 1:13 Binadamu hukomesha giza;
Huyatafutatafuta hata katika maeneo ya mbali,
Mawe ya madini katika giza, giza kuu.
4Hufukua shimo mbali na makao ya watu;
Husahauliwa na nyayo zipitazo;
Huning'inia mbali na watu, huyumbayumba huku na huko.
5Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula;
Na chini yake hupinduliwa kama kwa moto.
6Mawe yake ni mahali zipatikanapo yakuti;
Nayo ina mchanga wa dhahabu.
7Njia ile hapana ndege mkali aijuaye,
Wala jicho la tai halijaiona;
8Wanyama wakali wajivunao hawajaikanyaga,
Wala simba mkali hajaipita.
9Huunyoshea mwamba wa gumegume mkono wake;
Huipindua milima hata misingi yake.
10Hukata mifereji kati ya majabali;
Na jicho lake huona kila kito cha thamani.
11Hufunga vijito visichuruzike;
Na kitu kilichositirika hukifunua.
12 # Ayu 11:7,8; Zab 139:6; Mhu 7:24 Bali hekima itapatikana wapi?
Na mahali pa ufahamu ni wapi?
13 # Mit 3:15 Mwanadamu hajui thamani yake,
Wala haionekani katika nchi ya walio hai.
14 # Rum 11:33 Vilindi vyasema, Haimo ndani yangu;
Na bahari yasema, Haiko kwangu.
15 # Mit 3:13,14 Haipatikani kwa dhahabu,
Wala fedha haitapimwa iwe thamani yake.
16Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri,
Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti samawi.
17Dhahabu na vioo haviwezi kulinganishwa nayo;
Wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi.
18Havitatajwa fedhaluka wala bilauri;
Naam, kima cha hekima chapita marijani.
19Yakuti ya rangi ya manjano ya Kushi haitasawazishwa nayo,
Wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi.
20Basi hekima yatoka wapi?
Na mahali pa ufahamu ni wapi?
21Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai,
Na kusitirika na ndege wa angani.
22Uharibifu na Mauti husema,
Tumesikia habari zake kwa masikio yetu.
23 # Mdo 15:18; Ebr 4:13 Mungu ndiye aijuaye njia yake,
Naye anajua mahali pake.
24 # Mit 15:3 Maana anatazama hata miisho ya nchi,
Na kuona chini ya mbingu nzima.
25 # Zab 135:7 Apate kuufanyia upepo uzito wake;
Naam, anayapima maji kwa kipimo.
26 # Ayu 38:25; Zab 148:8; Yer 14:22 Hapo alipoiwekea mvua amri,
Na njia kwa umeme wa radi.
27Ndipo alipoiona na kuitangaza;
Aliithibitisha, naam, na kuichunguza.
28 # Zab 111:10; Mit 1:7; 9:10; Kum 29:29; 4:6 Kisha akamwambia mwanadamu,
Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima,
Na kujitenga na uovu ndio ufahamu.

Currently Selected:

Ayubu 28: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in