Yakobo 5
5
Onyo kwa matajiri wadhalimu
1 #
Lk 6:24
Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige mayowe kwa sababu ya mateso yenu yanayowajia. 2#Mt 6:19 Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3#Mit 16:27 Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho. 4#Kum 24:14-15; Law 19:13; Mal 3:5; Isa 5:9; Ayu 31:38-40 Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliokosa kuwalipa kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi. 5#Lk 16:19,25; Yer 12:3 Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejinenepesha mioyo yenu kama kwa siku ya kuchinjwa. 6Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi.
Uvumilivu katika mateso
7 #
Kum 11:14; Yoe 2:23; Zek 10:1; Yer 5:24; Lk 21:19; Ebr 10:36 Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. 8#Ebr 10:25; 1 The 2:16; 3:13 Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia.
9Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. 10#Mt 5:12 Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. 11#Ayu 1:21-22; 2:10; Zab 103:8; 111:4; Dan 12:12 Angalieni, twawaita heri wao waliostahimili. Mmesikia habari za kustahimili kwake Ayubu, kuona mwisho Bwana aliyomtendea, jinsi Bwana alivyo mwingi wa rehema na mwenye huruma.
12 #
Mt 5:34-37
Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali “ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, msije mkaanguka katika hukumu.
Sala ya imani
13 #
Zab 50:15; Kol 3:16 Kuna mtu miongoni mwenu anayeteseka? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. 14#Mk 6:13 Mtu wa kwenu amekuwa mgonjwa? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. 15#Mk 16:18 Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. 16Basi ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, ili mpate kuponywa. Sala yake mwenye haki ina nguvu nyingi, na hutenda mengi. 17#1 Fal 17:1; 18:1; Lk 4:25; Mdo 14:15 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia sawa na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18#1 Fal 18:42-45 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.
19 #
Gal 6:1
Ndugu zangu, mtu yeyote miongoni mwenu akipotoka mbali na kweli, na kurejeshwa na mtu mwingine; 20#Mit 10:12; 1 Pet 4:8; Zab 51:13 jueni ya kuwa yeye amrejeshaye mwenye dhambi hadi akatoka katika njia ya upotevu, ataokoa roho ya mwenye dhambi kutoka mauti, na kufunika wingi wa dhambi.
Currently Selected:
Yakobo 5: SRUV
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.