YouVersion Logo
Search Icon

Isaya 14

14
Kurudishwa kwa Yuda
1 # Zab 102:13,16; Isa 54:7,8; Yer 31:3,4,10,11; Zek 1:17; Isa 60:4,5,10 Maana BWANA atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo. 2Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya BWANA; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea.
Kuanguka kwa mfalme wa Babeli
3Tena itakuwa katika siku ile, ambayo BWANA atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa; 4#Isa 13:19; Hab 2:6 utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema,
Jinsi mdhalimu alivyokoma;
Jinsi ulivyokoma mji ule wenye ujeuri!
5BWANA amelivunja gongo la wabaya,
Fimbo ya enzi yao wenye kutawala.
6Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu,
Kwa mapigo yasiyokoma;
Aliyewatawala mataifa kwa hasira,
Ameadhibiwa asizuie mtu.
7Dunia yote inastarehe na kutulia;
Nao wanashangilia kwa kuimba.
8 # Isa 55:12; Eze 31:16 Naam, misonobari inakufurahia,
Na mierezi ya Lebanoni, ikisema,
Tokea wakati ulipolazwa chini wewe,
Hapana mkata miti aliyetujia.
9Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako,
Ili kukulaki utakapokuja;
Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako,
Naam, walio wakuu wote wa dunia;
Huwainua wafalme wote wa mataifa,
Watoke katika viti vyao vya enzi.
10Hao wote watajibu na kukuambia,
Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi!
Wewe nawe umekuwa kama sisi!
11Fahari yako imeshushwa hadi kuzimu,
Na sauti ya vinanda vyako;
Funza wametandazwa chini yako,
Na vidudu vinakufunika.
12 # Ufu 8:10; 9:1 Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,
Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi!
Jinsi ulivyokatwa kabisa,
Ewe uliyewaangusha mataifa!
13 # Omb 2:1; Dan 8:10; Ufu 12:4; Zab 48:2; Mt 11:23; Lk 10:15 Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni,
Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu;
Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano,
Katika pande za mwisho za kaskazini.
14 # Sef 2:15; 2 The 2:4 Nitapaa kupita vimo vya mawingu,
Nitafanana na yeye Aliye Juu.
15 # Isa 47:8; Eze 28:8,9; Mt 11:23; Mdo 12:23 Lakini utashushwa mpaka kuzimu;
Mpaka pande za mwisho za shimo.
16Wao wakuonao watakukazia macho,
Watakuangalia sana, wakisema,
Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia,
Huyu ndiye aliyetikisa falme;
17Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake;
Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?
18Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima,
Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe;
19Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako,
Kama chipukizi lililochukiza kabisa;
Kama vazi la wale waliouawa,
Wale waliochomwa kwa upanga,
Wale washukao mpaka misingi ya shimo;
Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu.
20Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi,
Kwa maana umeiharibu nchi yako,
Umewaua watu wako;
Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.
21 # Kut 20:5; Ayu 18:19; Mt 23:35 Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake.
Kwa sababu ya uovu wa baba zao;
Wasije wakainuka na kuitamalaki nchi,
Na kuujaza uso wa ulimwengu kwa miji.
22 # 1 Fal 14:10; Mit 10:7 Nami nitainuka, nishindane nao; asema BWANA wa majeshi; na katika Babeli nitang'oa jina na mabaki, mwana na mjukuu; asema BWANA. 23Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungunungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu; asema BWANA wa majeshi.
Utabiri juu ya Ashuru
24 # Isa 10:5-34; Nah 1:1—3:19; Sef 2:13-15 BWANA wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea; 25kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao. 26Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani kote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote. 27#2 Nya 20:6; Ayu 40:8; Isa 23:9; Yer 4:28 Maana BWANA wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?
Utabiri juu ya Ufilisti
28 # 2 Fal 16:20; 2 Nya 28:27 Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi.
29 # Yer 47:1-7; Eze 25:15-17; Yoe 3:4-8; Amo 1:6-8 Msifurahi, Enyi Wafilisti wote,
Kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika;
Maana katika shina la nyoka atatoka fira,
Na uzao wake ni joka la moto arukaye Sef 2:4-7; Zek 9:5-7
30Nao walio maskini kabisa watakula,
Na wahitaji watajilaza salama;
Nami nitatia shina lako kwa njaa,
Na mabaki yako watauawa.
31Piga yowe, Ee lango; lia, Ee mji;
Ee Ufilisti enyi wote, umeyeyuka kabisa;
Maana moshi unakuja toka kaskazini,
Wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.
32Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani? Ya kuwa BWANA ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake watapata kimbilio kwake.

Currently Selected:

Isaya 14: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in