YouVersion Logo
Search Icon

2 Wamakabayo 14

14
7. VITA NA NIKANO, JEMADARI WA DEMETRIO WA KWANZA. SIKU YA NIKANO
Alkimo ampinga Yuda
1Ikawa, baada ya miaka mitatu, Yuda na wenzake waliletewa habari ya kuwa Demetrio mwana wa Seleuko, pamoja na jeshi kubwa na merikebu nyingi, ameingia katika bandari ya Tripoli na kuishika nchi yote, 2baada ya kuwaua Antioko na mtunzaji wake Lisia. 3Basi, kulikuwa na mtu mmoja Alkimo, kuhani mkuu wa zamani, aliyejitia unajisi kwa hiari yake mwenyewe wakati wa matata. Huyu alijua ya kuwa yumo sasa katika hatari, wala hataweza tena kuiendea madhabahu takatifu. 4Kwa hiyo alimjia mfalme Demetrio, kunako mwaka mia moja na hamsini, akimletea zawadi ya taji la dhahabu na jani la mtende, pamoja na matawi ya mizeituni ya hekaluni. Siku ile hakusema neno. 5Lakini alipopata nafasi ya kutimiza kusudi lake ka kijinga – yaani, alipoitwa na Demetrio barazani na kuulizwa nia ya Wayahudi na makusudi yao – alijibu hivi: 6Wale Wayahudi waitwao Hasidimu, ambao kiongozi wao ni Yuda Makabayo, ndio wanaochochea vita na uasi, wasiiache nchi itulie. 7Ndiyo sababu mimi, niliyetwaliwa utukufu wangu wa asili, yaani ukuhani mkuu, nimekuja hapa, 8kwa sababu ya upendo wa kweli nilio nao kwa mambo ya mfalme, na nia yangu njema kwa raia wenzangu. Maana kwa matata ya wale niliowataja, taifa letu lote limo taabuni. 9Basi, mfalme, nakusihi, uzichunguze habari hizi, ufanye unavyoona vema kwa ajili ya nchi yetu na taifa letu lililodhikika, sawasawa na hisani yako uoneshayo kwa wote. 10Maana haiwezekani nchi ipate amani maadamu Yuda yu hai. 11Aliposema hayo, rafiki wengine wa mfalme waliomchukia Yuda walizidi kuichochea hasira ya mfalme; 12naye mara alimweka Nikano, ambaye alikuwa kwanza juu ya vikosi vya tembo, kuwa kiongozi wa Uyahudi, 13akampeleka na amri zilizoandikwa amwue Yuda na kuvunja jeshi lake, na kumfanya Alkimo kuhani mkuu wa hekalu lililo kuu. 14Ndipo wale wa Uyahudi walioshindwa na Yuda zamani walimwendea Nikano kwa haraka, wakitumaini kama dhiki na misiba ya Wayahudi itakuwa faida yao.
Nikano afanya urafiki na Yuda
15 # 1 Mak 7:27-28 Wayahudi walipopata habari za kuja kwa Nikano na mashambulio ya mataifa, walijitia mchanga kichwani, wakamsihi Yeye aliyewaweka watu wake imara milele, na kuutegemeza urithi wake daima, audhihirishe uweza wake. 16Kisha kwa amri ya kiongozi wao, waliondoka upesi wakapambana na adui penye mji uitwao Lesau. 17Simoni, ndugu yake Yuda, alikuwa amekwisha kupambana na Nikano, lakini alishikwa na fadhaa kwa wingi wa adui, akasimamishwa kwa muda. 18Hata hivi, Nikano, akipata sifa za ushujaa wa Yuda na watu wake, na nguvu yao katika vita walivyoipigania nchi yao, aliona shaka juu ya kupimana nguvu kwa vita. 19Kwa hiyo aliwatuma Posidonio na Theodoro na Matathia wapeane nao yamini. 20Masharti yakiisha fikiriwa, na kiongozi akiisha kuwaridhia watu wake, mapatano yalikubaliwa. 21Wakaweka siku ya kukutana peke yao. Machela ikachukuliwa mbele kutoka kila jeshi, na viti vya enzi vikawekwa. 22Yuda alisimamisha watu wenye silaha tayari katika mahali pa kufaa, isije labda ikatokea uhaini upande wa adui. Wakashauriana kama ilivyopasa. 23Nikano alikaa Yerusalemu kwa muda; hakufanya matata yoyote, bali alirudisha kwao ule umati wa watu waliojiunga naye. 24Alionana na Yuda kila mara, maana alimpenda kweli. 25Akamshauri aoe na kuzaa watoto. Basi alioa, akatulia, akafurahia maisha ya mjini.
Nikano awageuka Wayahudi
26Lakini Alkimo, alipoona walivyofanyana urafiki, alijipatia masharti ya yale mapatano yaliyofanyika, akamwendea Demetrio. Akamwarifu kwamba Nikano hana nia njema kwa ufalme, madhali amemweka yule mfitini Yuda awe mrithi wake. 27Mfalme akaghadhibika, na kwa jinsi alivyotiwa hasira kwa masingizio ya huyo mlaghai, alimwandikia Nikano kumwarifu ya kuwa yale mapatano hayampendezi na kumwamuru ampeleke Makabayo mfungwa mpaka Antiokia bila kukawia. 28Nikano alipopata maagizo hayo alitunduwaa; akafadhaika sana alipofikiri jinsi itakavyompasa kuyavunja mapatano waliyoyafanya, hali yule mtu hana kosa. 29Lakini kwa kuwa haiwezekani kuipinga amri ya mfalme, alingoja nafasi yake ya kuitimiza kwa hila. 30Makabayo, kwa upande wake, aliona ya kuwa Nikano hana mazungumzo naye kama kwanza, bali anaanza kumwonesha ukali, akafahamu ya kuwa ukimya huo ni dalili mbaya. Basi, akakusanya idadi kubwa ya wafuasi wake, wakaenda kujificha, Nikano asiwapate. 31#1 Mak 7:29-30 Basi huyo, alipofahamu ya kuwa ameshindwa kishujaa kwa werevu wa Yuda, alikwenda kwenye hekalu takatifu, lililo kuu, wakati makuhani walipokuwa wakitoa dhabihu za kawaida, akawaambia wamtolee yule mtu. 32Nao waliposema kwa kiapo ya kuwa hawajui yupo wapi mtu huyu anayemtafuta, 33alinyosha mkono wake wa kuume kwenye patakatifu akaapa kiapo hiki: Kama msipomtoa Yuda mfungwa kwangu, nitaiangusha nyumba hii ya Mungu hata nchi, na kuivunja madhabahu, na kujenga hapa hekalu la Dioniso watu wote walione. 34Akiisha kusema hayo aliondoka. Lakini makuhani, wakiinua mikono yao kuelekea mbinguni, walimwomba Yule anayelipigania taifa letu daima, wakisema: 35Ee BWANA, wewe usiye na haja ya ulimwengu umependa pawepo mahali patakatifu ili ukae miongoni mwetu. 36Basi, Ee BWANA mtakatifu, utakasaye vyote, uilinde safi daima nyumba hii iliyotakaswa hivi karibuni tu.
Razisi afia dini yake
37Kulikuwa na mtu mmoja, mzee wa Yerusalemu, jina lake Razisi, aliyeshtakiwa kwa Nikano. Alikuwa mpenda nchi yake, mtu mwenye sifa njema, aliyeitwa Baba wa Wayahudi kwa sababu ya hisani yake kwao. 38Katika siku za kwanza za matata alikuwa ameshtakiwa kwa kuwa ni Myahudi, naye alijihatarisha mwili wake na maisha yake kwa ushujaa mwingi kwa ajili ya Uyahudi. 39Basi, Nikano, akitaka kuudhihirisha uadui wake kwa Wayahudi, alipeleka askari zaidi ya mia tano kumkamata; 40maana kwa kumshika huyu alitaka kuwaumiza Wayahudi wote. 41Lakini askari walipokwisha kuuvunja mlango wa nje wakawa tayari kuutwaa mnara, wakiagiza moto wa kuichomea milango, yeye, akiona amezungukwa pande zote, aliuangukia upanga wake. 42Maana alipenda kufa kwa heshima kuliko kuanguka mikononi mwa hawa waovu na kutendwa jeuri isiyopatana na usharifu wake. 43Lakini kwa sababu ya haraka, pigo lake halikuingia sawasawa; kwa hiyo, watu walipokuwa wakijivurumisha mlangoni, alikimbilia ukutani akajitupa chini katikati ya mkutano. 44Hao wakarudi nyuma upesi, wakiacha nafasi, akaanguka chini, mahali pa wazi. 45Akasimama, angali yu hai, hasira yake ikiwaka kama moto; hata, ingawa damu yake ilikuwa ikibubujika, naye alijeruhiwa vibaya, alikimbia upesi katikati ya watu waliosongana, 46akasimama juu ya mwamba mrefu, ametokwa na damu karibu yote. Akang'oa matumbo yake, akayashika kwa mikono miwili, akawatupia makutano. Hivyo alikufa, akimwita Yeye aliye BWANA wa maisha na roho ayarudishe kwake tena.

Currently Selected:

2 Wamakabayo 14: SRUVDC

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in