YouVersion Logo
Search Icon

Mit 21:1-31

Mit 21:1-31 SUV

Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo. Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huipima mioyo. Kutenda haki na hukumu Humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka. Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa. Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali. Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu. Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa. Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri. Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili. Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi. Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza. Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima. Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao. Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake. Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi. Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi. Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya! Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo. Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya BWANA. Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini BWANA ndiye aletaye wokovu.