YouVersion Logo
Search Icon

Hes 16

16
Uhasama wa Kora, Dathani na Abiramu
1 # Yud 1:11 Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; 2#Hes 26:9nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; 3#Zab 106:16; Kut 19:6; 29:45nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yu kati yao; n’nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA? 4#Hes 20:6Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; 5#2 Tim 2:19; Law 21:6-12; Kut 28:1; 1 Sam 2:28; Zab 105:26; Law 10:3; Eze 40:46kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. 6Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; 7vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu BWANA atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi. 8Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; 9#1 Sam 18:23; Isa 7:13; Kum 10:8Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; 10tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? 11#Kut 16:8; 1 Kor 3:5Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha BWANA; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung’unikia? 12Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; 13#Kut 2:14; Mdo 7:27,35je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? 14#Kut 3:8; Law 20:24Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. 15#Mwa 4:4,5; 1 Sam 12:3; Mdo 20:33; 2 Kor 7:2Musa akakasirika sana, akamwambia BWANA. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. 16Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya BWANA kesho, wewe, na wao, na Haruni; 17mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za BWANA, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. 18Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. 19#Kut 16:7,10; Law 9:6,23Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote.
20Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 21#Mwa 19:17; Yer 51:6; Mdo 2:40; Ufu 18:4; Kut 32:10; 33:5; Zab 73:19; Isa 37:36Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja. 22#Ayu 12:10; Mhu 12:7; Isa 57:16; Zek 12:1; Ebr 12:9; 2 Sam 24:17; 1 Nya 21:17; Eze 18:20Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote? 23BWANA akasema na Musa, na kumwambia, 24Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu. 25Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye. 26#Mwa 19:12; Isa 52:11; Mdo 2:40; 2 Kor 6:17; Ufu 18:4Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. 27#Ayu 9:4; Mit 16:18Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. 28#Kut 3:12; Kum 18:22; Zek 2:9; Yer 23:16; Eze 13:17; Yn 5:30Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. 29#Kut 20:5; 32:34; Ayu 35:15; Isa 10:3; Yer 5:9; Omb 4:22Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. 30#Ayu 31:3; Isa 28:21; Zab 55:15; Ufu 9:2Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA 31#Hes 26:10; 27:3; Kum 11:6; Zab 106:17Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; 32#1 Nya 6:22nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. 33Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. 34Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. 35#Hes 11:1; Law 10:2; Zab 106:18Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.
36Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 37Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu; 38#Mit 20:2; Hab 2:10; Hes 17:10; 26:10; Eze 14:8; 1 Kor 10:11; 2 Pet 2:6vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuzihasiri nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za BWANA, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli. 39Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu; 40#Hes 3:38; 18:4-7; 1 Fal 13:1viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni awaye yote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za BWANA; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama BWANA alivyonena naye, kwa mkono wa Musa.
41 # Hes 14:2; Zab 106:13,26; Mt 5:11; Mdo 21:28; 2 Kor 6:8 Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung’unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa BWANA. 42#Kut 16:7,10; 24:16; 40:34; Law 9:23; Hes 14:10Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa BWANA ukaonekana. 43Na Musa na Haruni wakaenda hapo mbele ya hema ya kukutania. 44Naye BWANA akanena na Musa, na kumwambia, 45#Hes 20:6; 1 Nya 21:16; Mt 26:39Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi. 46#Law 10:6; Hes 1:53; 11:33; 18:5; Yos 7:1; 22:18; 1 Sam 6:19; 2 Sam 24:1; Zab 106:29; 1 Nya 27:24Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa BWANA; hiyo tauni imeanza. 47Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. 48#2 Sam 24:16,17,25; Ayu 33:24; Zab 106:30; Mt 20:28; 1 The 1:10; Ebr 7:24; Yak 5:16Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. 49Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. 50Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.

Currently Selected:

Hes 16: SUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy