Mt UTANGULIZI
UTANGULIZI
Mwandishi wa Injili ya Mathayo hataji jina lake. Lakini mapokeo kutoka jumuiya ya Wakristo wa karne za kwanza husema kuwa ni Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru na ambaye pengine huitwa Lawi wa Alfayo (9:9;10:3, Mk 2:14).
Mathayo alikusudia injili hii isomwe na Wakristo waliofahamu dini, mila na mazingira ya Kiyahudi. Shabaha yake ni kuonesha na kushuhudia kwamba Yesu ndiye Masihi ambaye walimtarajia, na ambaye angetimiza au kukamilisha zile ahadi za Mungu zilizo katika Agano la Kale. Kwa hiyo, picha tunayopewa na Mathayo juu ya Yesu ni kwamba yeye ndiye mfalme na Masihi (1:1; 19:28) ambaye kwake makusudi ya mpango au nia ya Mungu imefikia kilele chake: kwa nafsi yake Yesu Kristo Mungu mwenyewe amewajia wanadamu na kuwa kati yao (1:23). Kwake Yesu, Mungu ameanzisha jumuiya yake mpya (Israeli Mpya) ambayo ni wana wa Mungu.
Inaonekana kwamba kwa kuzingatia mada hiyo muhimu ya Imanueli (yaani “Mungu pamoja nasi”) Mathayo amepanga injili yake kana kwamba ingekuwa wasifu wa Yesu, na anafanya hivyo kwa kuweka pamoja katika sehemu tano mambo aliyofundisha Yesu; kila sehemu inaishia na njia maalumu ya kumalizia; kwa mfano: Ikawa Yesu alipoyamaliza maneno hayo… (7:28); “Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake…” (11:1); “Ikawa Yesu alipomaliza mifano hiyo…” (13:53), “Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo…” (19:1) na “Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote…” (26:1). Mafungu hayo matano ambayo yanahusu mada fulani dhahiri ndiyo haya:
Hotuba mlimani (sura 5:3–7:25);
Maagizo kuhusu utume wa Kikristo (sura 10:5-42);
Mifano ya ufalme wa mbinguni (sura 13:3-52);
Maisha ya kijamii ya Kikristo (sura 18:3-35);
Mwisho wa nyakati (sura 24:4–25:46).
Inaaminika kwamba injili zote nne hunukuu kutoka Agano la Kale ili kuonesha kwamba yaliyoaguliwa katika Agano la Kale yametimia katika Yesu Kristo. Lakini mwandishi Mathayo kwa namna ya pekee anazo nukuu tisa zaidi ambazo anazinukuu kutoka kwa ujumbe wa manabii, tena karibu neno kwa neno, kwa ajili ya walengwa wake waliojua dini ya Kiyahudi na desturi zao (1:22-23; 2:15; 2:17-18; 2:23; 4:14-16; 12:17-21; 13:15; 21:4-5; 27:9-10).
Mathayo anayo pia mafundisho mengine mengi ya Yesu na maneno aliyoyatumia ili kuwatia moyo wafuasi wake, kwa mfano: 8:20-22; 11:7-19,27-30; 12:48-50; 16:24-28; na 22:37-40, na pia maonyo au ole dhidi ya Waandishi na Mafarisayo (22:18-21; hasa 23:1-36), hata pia Yerusalemu (23:37-38) na miji mingine ya Galilaya (11:20-24).
Pamoja na hayo yote ni muhimu kukumbuka kwamba mada yenye uzito wa pekee katika injili hii ni juu ya ufalme wa Mungu, ambao Mathayo anauita kila mara “ufalme wa mbinguni” na ambao una hali mbili halisi: hali yake ya sasa (4:17; 12:20) na ya wakati ujao (16:28). Tangazo la Yesu juu ya kukaribia kwa ufalme wa Mungu ni wajibu ambao anawapa wafuasi wake kutangaza (10:7) wafuasi ambao baada ya yeye kufufuka kutoka kwa wafu aliwaahidi “tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata mwisho wa dunia” (28:20).
Currently Selected:
Mt UTANGULIZI: SUV
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.