Amo UTANGULIZI
UTANGULIZI
Jina Amosi maana yake ni “mzigo”. Amosi ni mzawa wa Tekoa, mji uliokuwa kama kilomita kumi na sita kusini mwa Yerusalemu.
Amosi alitoa unabii wakati wa utawala wa mfalme Yeroboamu wa pili wa Israeli na mfalme Uzia (au Azaria) wa Yuda (1:1). Nyakati za enzi ya wafalme hao zilikuwa kilele cha maendeleo na mafanikio. Mabadiliko makubwa yalikuwa mfumo wa jamii na uchumi wake. Kutoka kutegemea uchumi wa ukulima na ufugaji kuhamia mijini na kutegemea wafanya kazi na biashara. Hata hivyo, maskini wasiokuwa na uwezo kiuchumi waliongezeka, na kunyanyaswa. Pia, maovu kama magendo na rushwa yalishamiri. Vyombo vya kutetea na kulinda haki za raia havikuwa na uadilifu. Haki na kweli haikuwapo.
Amosi akawa nabii wa kwanza kukemea hali mbaya ya jamii. Ujumbe wake ulikuwa “tendeaneni haki maana Mungu wenu ni wa haki.” Aliwatetea wanyonge na kuwashutumu hadharani wafanya biashara wadanganyifu wenye dhulumu na ujeuri, viongozi wavunja sheria na wanaokula rushwa (2:6-7; 3:10; 5:12; 8:4-6). Kwa ujasiri alilaumu sikukuu za dini na waliotimiza kanuni za kutoa sadaka lakini wakiwatendea wenzao dhuluma na udhalimu (5:21-24, 8:3, 10).
Mungu alitaka wasikie ujumbe wa nabii ili watubu (5:1, 24). Maono matano yamekuwa kielelezo cha uvumilivu wa Mungu kwa taifa la Israeli. Hata hivyo hatimaye uvumilivu huo utafikia mwisho wake (7:1-9). Kwa kuwa mwisho umekaribia na taifa la Israeli limekuwa kaidi hakuna uwezekano wa kukwepa hukumu. Hivyo “Siku ya Bwana” itakuwa ni ya kuogofya (5:18) maana uovu wao ndio uliowaletea maangamizi (6:8-14; 7:8-9). Pamoja na ugumu wa watu kutotilia maanani maonyo ya Amosi (4:4-13) kuna matumaini kwa “mabaki” ya Yusufu kutohukumiwa (3:12, 5:15, 9:8-10). Mungu kwa neema yake atajenga taifa la “mabaki” upya na kulibariki (9:11-15).
Yaliyomo:
1. Hukumu ya Mungu kwa mataifa jirani ya Israeli na kwa Israeli yenyewe, Sura 1–2
2. Israeli yaonywa vikali sana, Sura 3–6
3. Maono ya hukumu, Sura 7:1–9:10
4. Matumaini ya kujengwa taifa upya, Sura 9:11–15
Currently Selected:
Amo UTANGULIZI: SUV
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.