YouVersion Logo
Search Icon

Marko 14

14
Kufa na kufufuka kwa Isa
(Marko 14:1–16:20)
Njama ya kumuua Isa
(Mathayo 26:1-5; Luka 22:1-2; Yohana 11:45-53)
1Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka#14:1 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri., na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Isa kwa hila na kumuua. 2Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.”
Isa apakwa mafuta huko Bethania
(Mathayo 26:6-13; Luka 7:35-38; Yohana 12:1-8)
3Isa alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo#14:3 aina ya manukato yaliyotengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Isa.
4Baadhi ya watu waliokuwa pale walikasirika na wakasemezana, “Upotevu huu wote wa manukato ni wa nini? 5Manukato haya yangeuzwa kwa zaidi ya dinari mia tatu#14:5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300., na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.
6Lakini Isa akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana. 7Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 8Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu. 9Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
Yuda akubali kumsaliti Isa
(Mathayo 26:14-16; Luka 22:3-6)
10Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Isa kwao. 11Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.
Isa ala Pasaka na wanafunzi wake
(Mathayo 26:17-25; Luka 22:7-14, 21-23; Yohana 13:21-30)
12Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Isa wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
13Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. 14Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 15Atawaonesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.”
16Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Isa alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
17Ilipofika jioni, Isa akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 18Walipoketi mezani wakila, Isa akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.”
19Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi, Bwana?”
20Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami. 21Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.”
Kuanzishwa kwa Chakula cha Bwana Isa
(Mathayo 26:26-30; Luka 22:14-20; 1 Wakorintho 11:23-25)
22Walipokuwa wanakula, Isa akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.”
23Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo.
24Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.”
26Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
Isa atabiri kuwa Petro atamkana
(Mathayo 26:31-35; Luka 22:31-34; Yohana 13:31-38)
27Isa akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:
“ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo watatawanyika.’#14:27 Zekaria 13:7
28Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
29Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.”
30Isa akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.”
31Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Isa aomba katika Bustani ya Gethsemane
(Mathayo 26:36-46; Luka 22:39-46)
32Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Isa akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.” 33Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika. 34Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”
35Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee. 36Akasema, “Abba#14:36 Abba ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba., Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”
37Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja? 38Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
39Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale. 40Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia.
41Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 42Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
Isa akamatwa
(Mathayo 26:47-56; Luka 22:47-53; Yohana 18:1-11)
43Isa alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa Torati, na wazee.
44Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.” 45Mara Yuda akamjia Isa na kusema, “Mwalimu.” Akambusu. 46Wale watu wakamkamata Isa, wakamweka chini ya ulinzi. 47Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
48Kisha Isa akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? 49Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.” 50Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
51Kijana mmoja, aliyekuwa amevaa nguo ya kitani pekee, alikuwa akimfuata Isa. Walipomkamata, 52alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
Isa mbele ya Baraza la Wayahudi
(Mathayo 26:57-68; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)
53Wakampeleka Isa kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa Torati wote wakakusanyika pamoja. 54Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.
55Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi#14:55 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Isa ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote. 56Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.
57Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema: 58“Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.
60Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Isa, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 61Lakini Isa akakaa kimya, hakusema neno lolote.
Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Al-Masihi#14:61 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”
62Isa akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
63Kuhani mkuu akayararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? 64Ninyi mmesikia alivyokufuru. Uamuzi wenu ni gani?”
Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo. 65Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.
Petro amkana Isa
(Mathayo 26:69-75; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)
66Petro alipokuwa bado yuko chini uani, tazama akaja mmoja wa wajakazi wa kuhani mkuu. 67Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Isa, Mnasiri.”
68Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.
69Yule mjakazi alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.” 70Lakini Petro akakana tena.
Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!” 71Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!”
72Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Isa alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.

Currently Selected:

Marko 14: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in