YouVersion Logo
Search Icon

Marko 11

11
Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Shangwe
(Mathayo 21:1-11; Luka 19:28-40; Yohana 12:12-19)
1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake, 2 akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 3 Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”
4 Wakaenda, wakamkuta mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. 5Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana-punda?” 6Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. 7Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. 8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. 9 Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,
“Hosana!”#11:9 Kiebrania kusema Okoa, basi likawa neno la shangwe.
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”
10 “Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”
“Hosana kwake yeye aliye juu!”
11 Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
Yesu Alaani Mtini Usiozaa
(Mathayo 21:18-19)
12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. 13Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. 14 Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.
Yesu Atakasa Hekalu
(Mathayo 21:12-17; Luka 19:45-48; Yohana 2:13-22)
15 Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, 16wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. 17 Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:
“ ‘Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote’?
Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ”
18 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote ulikuwa unashangazwa na mafundisho yake.
19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.
Mtini Ulionyauka
(Mathayo 21:20-22)
20 Asubuhi yake walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”
22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”
Swali Kuhusu Mamlaka Ya Yesu
(Mathayo 21:23-27; Luka 20:1-8)
27 Wakafika tena Yerusalemu, na Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wa watu wakamjia. 28Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”
29Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 30Niambieni, je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”
31Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 32 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’…” (Waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii wa kweli.)
33Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”
Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

Currently Selected:

Marko 11: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in