Mika 2
2
Mipango Ya Mwanadamu Na Ya Mungu
1 Ole kwa wale wapangao uovu,
kwa wale wafanyao shauri la hila vitandani mwao!
Kunapopambazuka wanalitimiza
kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.
2 Wanatamani mashamba na kuyakamata,
pia nyumba na kuzichukua.
Wanamlaghai mwanaume nyumba yake,
mwanadamu mwenzake urithi wake.
3 Kwa hiyo, Bwana asema:
“Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa,
ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe.
Hamtatembea tena kwa majivuno,
kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa.
4 Siku hiyo watu watawadhihaki,
watawafanyia mzaha
kwa wimbo huu wa maombolezo:
‘Tumeangamizwa kabisa;
mali ya watu wangu imegawanywa.
Ameninyangʼanya!
Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ”
5 Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la Bwana
wa kugawanya mashamba kwa kura.
Manabii Wa Uongo
6 Manabii wao husema, “Usitabiri.
Usitabiri kuhusu vitu hivi;
aibu haitatupata.”
7 Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo:
“Je, Roho wa Bwana amekasirika?
Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?”
“Je, maneno yangu hayamfanyii mema
yeye ambaye njia zake ni nyofu?
8Siku hizi watu wangu wameinuka
kama adui.
Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita
pasipo kujali,
kama watu warudio kutoka vitani.
9 Unawahamisha wanawake wa watu wangu
kutoka kwenye nyumba zao za kupendeza.
Unaondoa baraka yangu
kwa watoto wao milele.
10 Inuka, nenda zako!
Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia,
kwa sababu pametiwa unajisi,
pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena.
11 Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema,
‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’
angekuwa ndiye nabii
anayekubalika na watu hawa!
Ahadi Ya Ukombozi
12 “Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo,
Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli.
Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi,
kama kundi kwenye malisho yake,
mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu.
13 Yeye afunguaye njia atawatangulia;
watapita kwenye lango na kutoka nje.
Mfalme wao atawatangulia,
Bwana atakuwa kiongozi.”
Currently Selected:
Mika 2: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.