YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo 8

8
Mafundisho ya mifano na mazungumzo
(Mathayo 8–18)
Isa amtakasa mtu mwenye ukoma
(Marko 1:40-45; Luka 5:12-16)
1Isa aliposhuka kutoka mlimani, makundi ya watu wakamfuata. 2Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana#8:2 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., ukitaka, unaweza kunitakasa.”
3Isa akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake. 4Kisha Isa akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajioneshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Musa, ili kuwa ushuhuda kwao.”
Isa amponya mtumishi wa jemadari
(Luka 7:1-10)
5Isa alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, 6akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”
7Isa akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”
8Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia ndani ya nyumba yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 9Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliye chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
10Isa aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Ibrahimu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. 12Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa kilio na kusaga meno.”
13Kisha Isa akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona wakati ule ule.
Isa amponya mama mkwe wa Petro na pia watu wengi
(Marko 1:29-34; Luka 4:38-41)
14Isa alipoingia nyumbani mwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. 15Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.
16Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. 17Haya yalifanyika ili litimie neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya, kwamba:
“Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu
na akachukua magonjwa yetu.”#8:17 Isaya 53:4
Gharama ya kumfuata Isa
(Luka 9:57-62)
18Isa alipoona makundi mengi yamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke hadi ng’ambo ya ziwa. 19Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Isa na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata popote utakakoenda.”
20Naye Isa akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
21Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
22Lakini Isa akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”
Isa atuliza dhoruba
(Marko 4:35-41; Luka 8:22-25)
23Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. 24Ghafula, kukatokea dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Isa alikuwa amelala usingizi. 25Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”
26Naye Isa akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nayo bahari ikatulia kabisa.
27Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”
Watu wawili wenye pepo wachafu waponywa
(Marko 5:1-20; Luka 8:26-39)
28Walipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile. 29Wakapaza sauti wakisema, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu#8:29 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”
30Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakila. 31Wale pepo wachafu wakamsihi Isa, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.”
32Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji. 33Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu. 34Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Isa. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.

Currently Selected:

Mathayo 8: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in