Mathayo 16
16
Mafarisayo Wadai Ishara
(Marko 8:11-13; Luka 12:54-56)
1 Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.
2 Yesu akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ 3 Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati. 4 Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.
Chachu Ya Mafarisayo Na Masadukayo
(Marko 8:14-21)
5 Wanafunzi wake walipofika ngʼambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate. 6 Yesu akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”
7Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”
8 Yesu, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate? 9 Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya? 10 Au ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya? 11Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Petro Amkiri Yesu Kuwa Ni Mwana Wa Mungu
(Marko 8:27-30; Luka 9:18-21)
13 Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”
14 Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yohana Mbatizaji; wengine husema ni Eliya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”
15Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo,#16:16 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona,#16:17 Bar-Yona ni neno la Kiaramu, maana yake ni Mwana wa Yona. kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni. 18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kulishinda. 19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.” 20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
Yesu Anatabiri Juu Ya Kifo Chake
(Marko 8:31–9:1; Luka 9:22-27)
21 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.
22Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”
23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”
Currently Selected:
Mathayo 16: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.