YouVersion Logo
Search Icon

Mathayo 14

14
Yahya akatwa kichwa
(Marko 6:14-29; Luka 9:7-9)
1Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Isa, 2akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yahya; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
3Herode alikuwa amemkamata Yahya, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, 4kwa kuwa Yahya alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” 5Herode alitaka sana kumuua Yahya, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.
6Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana, 7kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. 8Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yahya kwenye sinia.” 9Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. 10Hivyo akaagiza Yahya akatwe kichwa mle gerezani. 11Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. 12Wanafunzi wa Yahya wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Isa.
Isa alisha wanaume 5,000
(Marko 6:30-44; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)
13Isa aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. 14Isa alipofika kando ya bahari, aliona makundi makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.
15Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makundi ya watu ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”
16Isa akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”
17Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”
18Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” 19Isa akaagiza umati wa watu wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia ule umati. 20Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.
Isa atembea juu ya maji
(Marko 6:45-52; Yohana 6:16-21)
22Mara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie katika mashua wamtangulie kwenda ng’ambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiaga ule umati. 23Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Isa alikuwa huko peke yake. 24Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.
25Wakati wa zamu ya nne ya usiku#14:25 yaani kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, Isa akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. 26Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.
27Lakini mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”
28Petro akamjibu, “Bwana Isa, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”
29Isa akamwambia, “Njoo.”
Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Isa. 30Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, akapaza sauti na kusema, “Bwana, niokoe!”
31Mara Isa akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”
32Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. 33Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Isa, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu#14:33 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..”
Isa awaponya wagonjwa Genesareti
(Marko 6:53-56)
34Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti. 35Watu wa eneo lile walipomtambua Isa, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote, 36wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

Currently Selected:

Mathayo 14: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in