Walawi 11
11
Vyakula Najisi Na Visivyo Najisi
(Kumbukumbu 14:3-21)
1 Bwana akawaambia Mose na Aroni, 2 “Waambieni Waisraeli: ‘Kati ya wanyama wote waishio juu ya nchi, hawa ndio mtakaowala: 3Mwaweza kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.
4“ ‘Kuna wanyama wengine ambao hucheua tu au wenye kwato zilizogawanyika tu, lakini hao kamwe msiwale. Ngamia ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; kwa kawaida ya ibada hiyo ni najisi kwenu. 5Pelele ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. 6 Sungura ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. 7 Naye nguruwe ingawa anazo kwato zilizogawanyika sehemu mbili, hacheui; huyo ni najisi kwenu. 8 Kamwe msile nyama yao wala kugusa mizoga yao; wao ni najisi kwenu.
9“ ‘Kuhusu viumbe wote wanaoishi ndani ya maji ya bahari na vijito, mtakula wale wote wenye mapezi na magamba. 10 Lakini viumbe wote ndani ya bahari au vijito wasio na mapezi na magamba, wakiwa miongoni mwa makundi au viumbe wote ndani ya maji, hao ni machukizo kwenu. 11 Nao watakuwa machukizo kwenu. Msile nyama yao, nayo mizoga yao itakuwa machukizo. 12Chochote kinachoishi ndani ya maji ambacho hakina mapezi na magamba kitakuwa chukizo kwenu.
13 “ ‘Wafuatao ndio ndege watakaokuwa machukizo kwenu, hivyo msiwale kwa sababu ni chukizo: tai, furukombe, kipungu, 14 mwewe mwekundu, aina zote za mwewe mweusi, 15 aina zote za kunguru, 16mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga, shakwe, aina zote za kipanga, 17bundi, mnandi, bundi mkubwa, 18 mumbi, mwari, nderi, 19 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.
20 “ ‘Wadudu wote warukao ambao hutembea kwa miguu minne watakuwa chukizo kwenu. 21Lakini wako viumbe wenye mabawa ambao hutembea kwa miguu minne mtakaowala: wale wenye vifundo katika miguu yao ya kurukaruka juu ya ardhi. 22Miongoni mwa hawa, mtakula nzige wa aina zote, senene, parare au panzi. 23Lakini viumbe wengine wote wenye mabawa na wenye miguu minne ni machukizo kwenu.
Wanyama Ambao Ni Najisi
24 “ ‘Mtajinajisi kwa wanyama hawa. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 25 Yeyote atakayebeba mizoga ya viumbe hawa ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
26“ ‘Kila mnyama mwenye ukwato ulioachana lakini haukugawanyika kabisa, au yule asiyecheua, huyo ni najisi kwenu; yeyote agusaye mzoga wowote wa hao atakuwa najisi. 27Miongoni mwa wanyama wote watembeao kwa miguu minne, wale watembeao kwa vitanga vyao ni najisi kwenu; yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 28 Yeyote atakayebeba mizoga yao ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Wanyama hawa ni najisi kwenu.
29“ ‘Kuhusu wanyama watambaao juu ya ardhi, hawa ni najisi kwenu: kicheche, panya, aina yoyote ya mijusi mikubwa, 30 guruguru, kenge, mijusi ya ukutani, goromoe na kinyonga. 31Hao wote watambaao juu ya ardhi ni najisi kwenu. Yeyote agusaye mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 32 Ikiwa mmoja wao atakufa na kuangukia juu ya kitu fulani, chombo hicho, hata kikiwa cha matumizi gani, kitakuwa najisi, kiwe kimetengenezwa kwa mti, nguo, ngozi au gunia. Kiweke ndani ya maji; kitakuwa najisi mpaka jioni, kisha kitakuwa safi tena. 33 Ikiwa mmoja wa wanyama aliyekufa ataangukia ndani ya chungu, kila kilichomo katika chungu hicho kitakuwa najisi, nawe ni lazima uvunje chungu hicho. 34Chakula chochote ambacho chaweza kuliwa lakini kikawa kimeingia maji kutoka kwenye chungu hicho ni najisi, na kitu chochote cha majimaji ambacho chaweza kunyweka kutoka kwenye chungu hicho ni najisi. 35Chochote ambacho mzoga wa mmojawapo utaangukia kitakuwa najisi. Jiko au chungu cha kupikia ni lazima kivunjwe. Ni najisi, nawe ni lazima uvihesabu kuwa najisi. 36Lakini chemchemi au kisima, mahali pa kuchota maji, patakuwa safi, lakini yeyote atakayegusa moja ya mizoga hii ni najisi. 37Kama mzoga ukianguka juu ya mbegu zozote ambazo ni za kupanda, zinabaki safi. 38Lakini kama mbegu imetiwa maji na mzoga ukaanguka juu yake, hiyo mbegu ni najisi kwenu.
39 “ ‘Kama mnyama ambaye mnaruhusiwa kumla akifa, yeyote atakayeugusa mzoga wake atakuwa najisi mpaka jioni. 40 Yeyote atakayekula sehemu ya mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni. Yeyote atakayebeba mzoga huo ni lazima afue nguo zake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
41“ ‘Kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi ni chukizo; kisiliwe. 42Msile kiumbe chochote kitambaacho juu ya ardhi, kiwe kitambaacho kwa tumbo lake, au kitambaacho kwa miguu minne au kwa miguu mingi; ni chukizo. 43 Msijitie unajisi kwa chochote katika viumbe hivi. Msijitie unajisi kwa viumbe hivyo au kutiwa unajisi navyo. 44 Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; jitakaseni mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu. Msijitie unajisi wenyewe kwa kiumbe chochote kile kiendacho juu ya ardhi. 45 Mimi ndimi Bwana niliyewapandisha mtoke Misri ili niwe Mungu wenu. Kwa hiyo kuweni watakatifu kwa sababu Mimi ni mtakatifu.
46“ ‘Haya ndiyo masharti kuhusu wanyama, ndege, kila kiumbe hai kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kiendacho juu ya ardhi. 47 Ni lazima mpambanue kati ya kilicho najisi na kilicho safi, kati ya viumbe hai vinavyoweza kuliwa na vile visivyoweza kuliwa.’ ”
Currently Selected:
Walawi 11: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.