YouVersion Logo
Search Icon

Yeremia 28

28
Hanania Nabii Wa Uongo
1 Katika mwezi wa tano wa mwaka ule ule, yaani mwaka wa nne, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, nabii Hanania mwana wa Azuri, ambaye alitoka Gibeoni, akaniambia katika nyumba ya Bwana mbele ya makuhani na watu wote: 2 “Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli. 3 Katika muda wa miaka miwili nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Bwana ambavyo Nebukadneza mfalme wa Babeli aliviondoa kutoka hapa na kuvipeleka Babeli. 4 Pia nitamrudisha mahali hapa Yekonia#28:4 Yekonia au Konia ni jina jingine la Yehoyakini. mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na wote waliohamishwa kutoka Yuda ambao walikwenda Babeli,’ asema Bwana, ‘kwa kuwa nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.’ ”
5Ndipo nabii Yeremia akamjibu nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama ndani ya nyumba ya Bwana. 6 Akasema, “Amen! Bwana na afanye hivyo! Bwana na ayatimize maneno uliyotoa unabii kwa kuvirudisha mahali hapa kutoka Babeli vyombo vya nyumba ya Bwana pamoja na wote waliohamishwa. 7Hata hivyo, nisikilize nikuambie yale nitakayoyasema masikioni mwako na masikioni mwa watu hawa wote: 8 Tangu mwanzo, manabii waliokutangulia wewe na mimi walitabiri vita, maafa na tauni dhidi ya nchi nyingi na falme kubwa. 9 Lakini nabii atakayetabiri amani atatambuliwa kuwa kweli ametumwa na Bwana ikiwa unabii wake utatimia.”
10 Kisha nabii Hanania akaiondoa nira iliyokuwa shingoni mwa Yeremia na kuivunja, 11 naye akasema mbele ya watu wote, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Vivi hivi ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadneza mfalme wa Babeli kutoka kwenye shingo za mataifa katika muda huu wa miaka miwili.’ ” Alipofanya hivi, nabii Yeremia akaondoka zake.
12Kitambo kidogo baada ya nabii Hanania kuivunja nira kutoka shingo ya nabii Yeremia, neno la Bwana likamjia Yeremia: 13“Nenda ukamwambie Hanania, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Umevunja nira ya mti, lakini badala yake utapata nira ya chuma. 14 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Nitaweka nira ya chuma kwenye shingo za mataifa haya yote ili kufanya yamtumikie Nebukadneza mfalme wa Babeli, nao watamtumikia. Nitampa kutawala hata wanyama wa mwituni.’ ”
15 Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, “Sikiliza Hanania! Bwana hajakutuma, lakini wewe umelishawishi taifa hili kuamini uongo. 16 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: ‘Hivi karibuni nitakuondoa kutoka juu ya uso wa dunia. Mwaka huu utakufa, kwa sababu umetangaza uasi dhidi ya Bwana.’ ”
17 Katika mwezi wa saba wa mwaka ule ule, nabii Hanania akafa.

Currently Selected:

Yeremia 28: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

Video for Yeremia 28