YouVersion Logo
Search Icon

Waamuzi Utangulizi

Utangulizi
Jina la kitabu hiki limetokana na viongozi waliojulikana kama Waamuzi ambao Mungu aliwainua kuongoza nchi ya Israeli. Hii ilitokana na kupotoka kwingi na kurudi nyuma kwa wana wa Israeli baada ya kifo cha Yoshua. Kwa sababu yeye alikuwa amewachagua kuwa watu wake, ambao kupitia kwao watu wote wangeweza kujua upendo wa Mungu, basi Mungu asingewaacha waanguke kabisa chini ya uonevu wa adui zao. Kitabu hiki kinaelezea habari za Waisraeli kwa kipindi kati ya kifo cha Yoshua na huduma ya Samweli.
Mungu alikuwa amewasaidia Waisraeli kuishinda na kuiteka Kanaani, ambako ndani yake yaliishi mataifa mengi maovu. Lakini walikuwa katika hatari ya kuipoteza hii Nchi ya Ahadi kwa sababu walianza kumwasi Mungu. Walipomrudia Mungu, naye Mungu aliwainulia Waamuzi wa kuwaokoa kutoka mikononi mwa adui zao, na kuwarudisha tena katika njia na kusudi lake, na kuwaongoza. Hivyo kipindi hiki kilijulikana kwa mashujaa walioitwa Waamuzi ambao ndio walioongoza makabila ya Israeli. Jumla ya waamuzi kumi na wanne wameorodheshwa kuwa waliiongoza Israeli katika kitabu hiki. Waliojulikana zaidi walikuwa Yefta, Debora, Gideoni na Samsoni.
Mataifa yaliyowaonea Waisraeli wakati wa kipindi hiki cha Waamuzi yalikuwa: Wakaldayo, Wamoabu, Wakanaani, Wamidiani, Waamoni na Wafilisti. Kipindi hiki cha Waamuzi kilidumu kwa miaka 410 kikitazamwa na vile matukio yalivyofuatana.
Mwandishi
Mwandishi wa kitabu hiki hajulikani ni nani, lakini mapokeo ya Kiyahudi yanasema ni Samweli.
Kusudi
Ni kuonyesha kwamba hukumu ya Mungu juu ya dhambi ni lazima, na pia kuwasamahe na kuwarudisha waliotubu katika uhusiano wake ni lazima.
Mahali
Nchi ya Kanaani ambayo baadaye iliitwa Israeli.
Tarehe
Wakati kitabu hiki kiliandikwa haujulikani.
Wahusika Wakuu
Othnieli, Ehudi, Debora, Gideoni, Abimeleki, Yefta, Samsoni na Delila.
Wazo Kuu
Baada ya Yoshua kufariki, Waisraeli walikuwa wakiinuka walipompata kiongozi na baada ya kiongozi huyo kufariki walipotoka na kuangukia mikononi mwa maadui zao. Walipomlilia Mungu aliwainulia mwamuzi, ambaye aliwaongoza na kuwapa ushindi.
Mambo Muhimu
Mambo mawili muhimu katika kitabu cha Waamuzi ni vile Waisraeli waligandamizwa na mataifa jirani kwa sababu ya kumwasi Mungu, na vile Mungu aliwakomboa kutoka kwa watesi wao baada ya kutubu na kumrudia.
Mgawanyo
Waisraeli kushindwa kuyafukuza kabisa mataifa yaliyokuwa nchi ya Kanaani (1:1–3:6)
Waamuzi kuwakomboa Waisraeli (3:7–16:31)
Waisraeli kuanguka kiroho, kimaadili na kisiasa (17:1–21:25).

Currently Selected:

Waamuzi Utangulizi: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in