Yakobo 3
3
Kuufuga Ulimi
1 Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi. 2 Sisi sote tunajikwaa katika mambo mengi. Ikiwa mtu yeyote hakosei kamwe katika yale anayosema, yeye ni mkamilifu, naye anaweza kuuzuia pia na mwili wake wote.
3 Tunapotia lijamu kwenye vinywa vya farasi ili kuwafanya watutii, tunaweza kuigeuza miili yao yote. 4Au angalia pia meli, ingawa ni kubwa sana, nazo huchukuliwa na upepo mkali, lakini hugeuzwa kwa usukani mdogo sana, kokote anakotaka nahodha. 5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! 6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.
7Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini vinafugika na vimefugwa na binadamu, 8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.
9 Kwa ulimi tunamhimidi Bwana, yaani Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. 10Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo. 11 Je, chemchemi yaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi? 12 Je, ndugu zangu, mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.
Aina Mbili Za Hekima
13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima. 14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli. 15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni, bali ni ya kidunia, isiyo ya kiroho, na ya kishetani. 16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi, ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.
17Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, tena ni ya upole, iliyo tayari kusikiliza wengine kwa unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki. 18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.
Currently Selected:
Yakobo 3: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.