YouVersion Logo
Search Icon

2 Wafalme 24

24
1 Wakati wa utawala wa Yehoyakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi, naye Yehoyakimu akawa mtumwa wake kwa miaka mitatu. Lakini hatimaye akabadili mawazo yake na kuasi dhidi ya Nebukadneza. 2 Bwana akatuma wavamiaji wa Wakaldayo, Waaramu, Wamoabu na Waamoni ili kumshambulia. Aliwatuma kuiangamiza Yuda sawasawa na neno la Bwana lililosemwa na watumishi wake manabii. 3 Hakika mambo haya yalitokea Yuda kulingana na agizo la Bwana, ili kuwaondoa kutoka machoni pake kwa sababu ya dhambi za Manase na yote aliyoyafanya, 4 ikiwa ni pamoja na kumwaga damu isiyo na hatia. Kwa kuwa aliijaza Yerusalemu kwa damu isiyo na hatia, naye Bwana hakuwa radhi kusamehe.
5 Matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 6 Yehoyakimu akalala pamoja na baba zake. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
7 Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa sababu mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa himaya yake yote, kuanzia Kijito cha Misri hadi Mto Frati.
Yehoyakini Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 36:9-10)
8 Yehoyakini alikuwa na miaka kumi na minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu. Jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu. 9 Akafanya maovu machoni pa Bwana, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
10 Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja ili kuishambulia Yerusalemu, nao wakaizunguka kwa jeshi. 11Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzunguka kwa jeshi. 12 Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza.
Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa. 13 Kama vile Bwana alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la Bwana na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana. 14 Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na mashujaa, watu wenye ustadi na ufundi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana ndio tu waliobaki katika nchi.
15 Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi. 16 Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli mashujaa elfu saba, wenye nguvu na wanaofaa kupigana vita, na watu wenye ustadi na mafundi elfu moja. 17 Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake, na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.
Sedekia Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 36:11-12; Yeremia 52:1-3)
18 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna. 19Alifanya maovu machoni pa Bwana, kama alivyofanya Yehoyakimu. 20Ilikuwa ni kwa sababu ya hasira ya Bwana haya yote yalitokea Yerusalemu na Yuda, naye mwishoni akawaondoa mbele zake.
Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.

Currently Selected:

2 Wafalme 24: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in