2 Wafalme 14
14
Amazia Mfalme Wa Yuda
(2 Nyakati 25)
1Katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani, kutoka Yerusalemu. 3Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.
4 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
5 Baada ya ufalme kuimarika mikononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake. 6 Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose ambako Bwana aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
7 Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.
8Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, “Njoo, tuonane uso kwa uso.”
9 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli akamjibu Amazia mfalme wa Yuda: “Mbaruti uliokuwa Lebanoni ulituma ujumbe kwa mwerezi uliokuwa Lebanoni, ‘Mtoe binti yako aolewe na mwanangu.’ Kisha mnyama wa mwituni aliyekuwa Lebanoni akaja na kuukanyaga ule mbaruti. 10 Hakika umeishinda Edomu, na sasa unajivuna. Jisifu katika ushindi wako, lakini kaa nyumbani kwako! Kwa nini unachokoza na kujiletea anguko lako mwenyewe na la Yuda pia?”
11 Hata hivyo, Amazia hakusikia, hivyo Yehoashi mfalme wa Israeli akashambulia. Yeye na Amazia mfalme wa Yuda wakakutana uso kwa uso huko Beth-Shemeshi katika Yuda. 12 Yuda ikashindwa na Israeli, na kila mtu akakimbilia nyumbani kwake. 13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yoashi, mwana wa Ahazia, huko Beth-Shemeshi. Kisha Yehoashi akaenda Yerusalemu na kuubomoa ukuta wa Yerusalemu kuanzia Lango la Efraimu hadi Lango la Pembeni, sehemu yenye urefu wa kama dhiraa 400.#14:13 Dhiraa 400 ni sawa na mita 180. 14Akachukua dhahabu yote na fedha na vyombo vyote vilivyopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina zote za jumba la mfalme. Akachukua pia mateka na akarudi Samaria.
15 Matukio mengine ya utawala wa Yehoashi, aliyoyafanya na mafanikio yake, pamoja na vita vyake dhidi ya Amazia mfalme wa Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 16Yehoashi akalala pamoja na baba zake, akazikwa Samaria pamoja na wafalme wa Israeli, naye Yeroboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
17Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya kifo cha Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli. 18Matukio mengine ya utawala wa Amazia, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
19 Wakafanya shauri baya dhidi ya Amazia huko Yerusalemu, naye akakimbilia Lakishi, lakini wakawatuma watu wamfuatilie huko Lakishi, nao wakamuulia huko. 20Akarudishwa kwa farasi na akazikwa huko Yerusalemu pamoja na baba zake katika Mji wa Daudi.
21 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria#14:21 Azaria pia aliitwa Uzia. aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, na kumfanya mfalme mahali pa baba yake Amazia. 22Ndiye aliijenga tena Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.
Yeroboamu Wa Pili Mfalme Wa Israeli
23 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, naye akatawala kwa miaka arobaini na mmoja. 24Akafanya maovu machoni pa Bwana, na hakuacha dhambi hata moja ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alikuwa amesababisha Israeli kuzitenda. 25 Ndiye alirudishia mipaka ya Israeli kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bahari ya Araba, sawasawa na neno la Bwana, Mungu wa Israeli, lililosemwa kupitia mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii kutoka Gath-Heferi.
26 Bwana alikuwa ameona jinsi kila mmoja katika Israeli, awe mtumwa au aliye huru, alivyoteseka kwa uchungu; hapakuwepo na yeyote wa kuwasaidia. 27 Kwa kuwa Bwana alikuwa hajasema kuwa atafuta jina la Israeli chini ya mbingu, akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
28 Kwa matukio mengine ya utawala wa Yeroboamu, yote aliyoyafanya na mafanikio yake ya kijeshi, ikiwa ni pamoja na jinsi alivyorudisha Dameski na Hamathi kwa Israeli, ambayo ilikuwa mali ya Yuda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 29Yeroboamu akalala pamoja na baba zake, wafalme wa Israeli. Naye Zekaria mwanawe akawa mfalme baada yake.
Currently Selected:
2 Wafalme 14: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Neno: Biblia Takatifu™ Neno™
Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Version™
Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc.
Used with Permission. All Rights Reserved Worldwide.