YouVersion Logo
Search Icon

1 Wafalme 12

12
Israeli Yaasi Dhidi Ya Rehoboamu
(2 Nyakati 10:1-19)
1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Waisraeli wote walikuwa wamekwenda huko kumfanya yeye kuwa mfalme. 2 Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia hili (alikuwa bado yuko Misri alikokuwa amekimbilia awe mbali na Mfalme Solomoni), akarudi kutoka Misri. 3Kwa hiyo wakatuma watu kumwita Yeroboamu, yeye na kusanyiko lote la Israeli wakamwendea Rehoboamu na kumwambia, 4 “Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini sasa tupunguzie kazi za kikatili na nira nzito aliyoweka juu yetu, nasi tutakutumikia.”
5Rehoboamu akajibu, “Nendeni kwa muda wa siku tatu na kisha mnirudie.” Basi watu wakaenda zao.
6 Kisha Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee ambao walimtumikia Solomoni baba yake wakati wa uhai wake akawauliza, “Mnanishauri nini katika kuwajibu watu hawa?”
7 Wakajibu, “Kama leo utakuwa mtumishi wa watu hawa na kuwahudumia na kuwapa jibu linaloridhisha, watakuwa watumishi wako daima.”
8 Lakini Rehoboamu akakataa shauri alilopewa na wazee na akataka ushauri kwa vijana wanaume rika lake waliokuwa wakimtumikia. 9Akawauliza, “Ninyi ushauri wenu ni nini? Tutawajibuje watu hawa wanaoniambia, ‘Ifanye nyepesi nira baba yako aliyoweka juu yetu?’ ”
10Wale vijana wa rika lake wakamjibu, “Waambie watu hawa waliokuambia, ‘Baba yako aliweka nira nzito juu yetu, lakini ifanye nira yetu nyepesi,’ kuwa, ‘Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 11Baba yangu aliweka nira nzito juu yenu, mimi nitaifanya hata iwe nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.’ ”
12Siku tatu baadaye, Yeroboamu na watu wote wakamrudia Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amesema, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” 13Mfalme akawajibu watu kwa ukatili. Akikataa shauri alilopewa na wazee, 14 akafuata shauri la vijana wa rika lake na kusema, “Baba yangu alifanya nira yenu kuwa nzito, mimi nitaifanya kuwa nzito zaidi. Baba yangu aliwachapa kwa mijeledi, mimi nitawachapa kwa nge.” 15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza watu, kwa kuwa jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili kutimiza neno ambalo Bwana alikuwa amenena kwa Yeroboamu mwana wa Nebati kupitia Ahiya Mshiloni.
16 Israeli wote walipoona kuwa mfalme amekataa kuwasikiliza, wakamjibu mfalme:
“Tuna fungu gani kwa Daudi?
Sisi hatuna urithi kwa mwana wa Yese.
Nendeni kwenye mahema yenu, ee Israeli!
Angalia nyumba yako mwenyewe, ee Daudi!”
Hivyo Waisraeli wakaenda kwenye mahema yao. 17 Lakini kwa habari ya Waisraeli waliokuwa wakiishi katika miji ya Yuda, Rehoboamu akaendelea kuwatawala bado.
18 Mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa msimamizi wa wale waliofanya kazi ngumu kwa kulazimishwa, lakini Israeli wote wakampiga kwa mawe hadi akafa. Hata hivyo, Mfalme Rehoboamu, akafanikiwa kuingia kwenye gari lake na kutorokea Yerusalemu. 19 Hivyo Israeli wakaasi dhidi ya nyumba ya Daudi hadi leo.
20 Waisraeli wote waliposikia kwamba Yeroboamu amerudi, wakatuma watu na kumwita kwenye kusanyiko na kumfanya mfalme juu ya Israeli yote. Ni kabila la Yuda peke yake lililobaki kuwa tiifu kwa nyumba ya Daudi.
21 Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda na kabila la Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.
22 Lakini neno hili la Mungu likamjia Shemaya mtu wa Mungu: 23“Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, na nyumba yote ya Yuda na Benyamini, na watu wengine wote, 24‘Hili ndilo asemalo Bwana: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu, Waisraeli. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na kurudi nyumbani, kama Bwana alivyokuwa ameagiza.
Ndama Wa Dhahabu Huko Betheli Na Dani
25 Kisha Yeroboamu akajenga Shekemu akaizungushia ngome katika nchi ya vilima ya Efraimu na akaishi huko. Akatoka huko, akaenda akajenga Penueli.#12:25 Jina lingine ni Penieli kwa Kiebrania.
26Yeroboamu akawaza moyoni mwake, “Sasa inawezekana ufalme ukarudi katika nyumba ya Daudi. 27 Kama watu hawa watapanda kwenda kutoa dhabihu katika Hekalu la Bwana huko Yerusalemu, mioyo yao itamrudia bwana wao, Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua mimi na kurudi kwa Mfalme Rehoboamu.”
28 Baada ya kutafuta shauri, mfalme akatengeneza ndama wawili wa dhahabu. Akawaambia watu, “Ni gharama kubwa kwenu kukwea kwenda Yerusalemu. Hii hapa miungu yenu, ee Israeli, iliyowapandisha kutoka Misri.” 29 Ndama mmoja akamweka Betheli na mwingine Dani. 30 Nalo jambo hili likawa dhambi, watu wakawa wanaenda hadi Dani kumwabudu huyo aliyewekwa huko.
31 Yeroboamu akajenga madhabahu mahali pa juu pa kuabudia miungu na kuwateua makuhani kutoka watu wa aina zote, ijapokuwa hawakuwa Walawi. 32 Pia Yeroboamu akaweka sikukuu katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, kama sikukuu iliyokuwa ikifanyika huko Yuda, na akatoa dhabihu juu ya madhabahu. Akafanya hivyo huko Betheli akitoa dhabihu kwa ndama alizotengeneza. Huko Betheli akawaweka makuhani, na pia katika sehemu za juu za kuabudia miungu alizozitengeneza. 33 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouchagua mwenyewe, alitoa dhabihu juu ya madhabahu aliyokuwa amejenga huko Betheli. Kwa hiyo akaweka sikukuu kwa ajili ya Waisraeli na akapanda madhabahuni kutoa sadaka.

Currently Selected:

1 Wafalme 12: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in