2 Kor 7:1-10
Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu. Tupeni nafasi mioyoni mwenu. Hatukumdhulumu mtu ye yote, wala kumharibu mtu, wala kumkaramkia mtu. Sisemi neno hilo ili niwahukumu ninyi kuwa na hatia; kwa maana nimetangulia kusema, ya kwamba ninyi mmo mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja, na kuishi pamoja. Ninao ujasiri mwingi kwenu; naona fahari kuu juu yenu. Nimejaa faraja, katika dhiki yetu yote nimejaa furaha ya kupita kiasi. Kwa maana hata tulipokuwa tumefika Makedonia miili yetu haikupata nafuu; bali tulidhikika kote kote; nje palikuwa na vita, ndani hofu. Lakini Mungu, mwenye kuwafariji wanyonge, alitufariji kwa kuja kwake Tito. Wala si kwa kuja kwake tu, bali kwa zile faraja nazo alizofarijiwa kwenu, akituarifu habari ya shauku yenu, na maombolezo yenu, na bidii yenu kwa ajili yangu, hata nikazidi kufurahi. Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu. Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.
2 Kor 7:1-10