1 Nya 29:10-20
Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye.
1 Nya 29:10-20