Zekaria 8:9-17
Zekaria 8:9-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Jipeni moyo! Sasa mnayasikia maneno ambayo mlitangaziwa na manabii wakati ulipowekwa msingi wa hekalu langu, kulijenga upya. Kabla ya wakati huo, watu hawakupata mshahara kwa kazi zao wala kwa kukodisha mnyama. Hamkuwa na usalama kwa sababu ya adui zenu, maana nilisababisha uhasama kati ya watu wote. Lakini sasa sitawatendea hao watu wa taifa hili waliosalia kama hapo zamani. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Sasa nitaleta tena amani duniani, mvua itanyesha kama kawaida, ardhi itatoa mazao, na mizabibu itazaa kwa wingi. Nitawapa watu waliosalia wa taifa hili hayo yote yawe mali yao. Enyi watu wa Yuda na watu wa Israeli! Wakati uliopita nyinyi mlionekana kuwa watu waliolaaniwa kati ya watu wa mataifa. Lakini sasa mimi nitawaokoeni, nanyi mtakuwa watu waliobarikiwa. Basi, msiogope tena, bali jipeni moyo!” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kama nilivyokusudia kuwatendea nyinyi maovu kwa sababu wazee wenu walinikasirisha, na wala sikuwaonea huruma, vivyo hivyo nimekusudia kuutendea wema mji wa Yerusalemu na watu wa Yuda. Basi, msiogope. Hivi ndivyo mnavyopaswa kufanya: Kila mmoja wenu na amwambie mwenzake ukweli. Mahakama yenu daima na yatoe hukumu za haki ziletazo amani. Mtu yeyote miongoni mwenu asikusudie kutenda uovu dhidi ya mwenzake, wala msiape uongo, maana nayachukia sana matendo hayo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Zekaria 8:9-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA wa majeshi asema hivi, Mikono yenu na iwe hodari, ninyi mnaosikia siku hizi maneno haya kwa vinywa vya manabii, waliokuwapo siku hiyo ulipowekwa msingi wa nyumba ya BWANA wa majeshi; yaani, hekalu hilo; ili lijengwe. Maana kabla ya siku zile hapakuwa na ijara kwa mwanadamu, wala hapakuwa na ijara kwa mnyama; wala hapakuwa na amani kwake yeye aliyetoka, wala kwake yeye aliyeingia, kwa sababu ya adui; nami nilimwacha kila mtu kugombana na jirani yake. Lakini sasa sitakuwa kwa mabaki ya watu hawa kama nilivyokuwa siku zile za kwanza, asema BWANA wa majeshi. Kwa maana itakuwako mbegu ya amani; mzabibu utatoa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na hizo mbingu zitatoa umande wake; nami nitawarithisha mabaki ya watu hawa vitu hivi vyote. Kisha itakuwa, kama vile mlivyokuwa laana katika mataifa, Ee nyumba ya Yuda, na nyumba ya Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka; msiogope, lakini mikono yenu na iwe hodari. Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Kama vile nilivyoazimia kuwatenda ninyi mabaya, baba zenu waliponikasirisha, asema BWANA wa majeshi, wala mimi sikujuta; vivyo hivyo nimeazimia katika siku hizi kuutendea Yerusalemu mema, na nyumba ya Yuda pia; msiogope. Haya ndiyo mtakayoyatenda; kila mtu na aseme ukweli na jirani yake; katika malango yenu toeni hukumu za kweli na ziletazo amani; wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu ya jirani yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo niyachukiayo, asema BWANA.
Zekaria 8:9-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA wa majeshi asema hivi, Mikono yenu na iwe hodari, ninyi mnaosikia siku hizi maneno haya kwa vinywa vya manabii, waliokuwapo siku hiyo ulipowekwa msingi wa nyumba ya BWANA wa majeshi; yaani, hekalu hilo; ili lijengwe. Maana kabla ya siku zile hapakuwa na ijara kwa mwanadamu, wala hapakuwa na ijara kwa mnyama; wala hapakuwa na amani kwake yeye aliyetoka, wala kwake yeye aliyeingia, kwa sababu ya adui; nami nalimwacha kila mtu kugombana na jirani yake. Lakini sasa sitakuwa kwa mabaki ya watu hawa kama nilivyokuwa siku zile za kwanza, asema BWANA wa majeshi. Kwa maana itakuwako mbegu ya amani; mzabibu utatoa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na hizo mbingu zitatoa umande wake; nami nitawarithisha mabaki ya watu hawa vitu hivi vyote. Kisha itakuwa, kama vile mlivyokuwa laana katika mataifa, Ee nyumba ya Yuda, na nyumba ya Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka; msiogope, lakini mikono yenu na iwe hodari. Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Kama vile nilivyoazimia kuwatenda ninyi mabaya, baba zenu waliponikasirisha, asema BWANA wa majeshi, wala mimi sikujuta; vivyo hivyo nimeazimia katika siku hizi kuutendea Yerusalemu mema, na nyumba ya Yuda pia; msiogope. Haya ndiyo mtakayoyatenda; kila mtu na aseme kweli na jirani yake; hukumuni kweli na hukumu ya amani malangoni mwenu; wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu ya jirani yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo niyachukiayo, asema BWANA.
Zekaria 8:9-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Ninyi ambao sasa mnasikia maneno haya yanayozungumzwa na manabii ambao walikuwepo wakati wa kuwekwa kwa msingi wa nyumba ya BWANA Mwenye Nguvu Zote, mikono yenu na iwe na nguvu ili Hekalu liweze kujengwa. Kabla ya wakati huo, hapakuwepo na ujira kwa mtu wala mnyama. Hakuna mtu aliyeweza kufanya shughuli yake kwa usalama kwa sababu ya adui yake, kwa kuwa nilikuwa nimemfanya kila mtu adui wa jirani yake. Lakini sasa sitawatendea mabaki ya watu hawa kama nilivyowatenda zamani,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Mbegu itakua vizuri, mzabibu utazaa matunda yake, ardhi itatoa mazao yake, na mbingu zitadondosha umande wake. Vitu hivi vyote nitawapa mabaki ya watu kama urithi wao. Jinsi mlivyokuwa kitu cha laana katikati ya mataifa, ee Yuda na Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka. Msiogope, bali iacheni mikono yenu iwe na nguvu.” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Kama nilivyokuwa nimekusudia kuleta maangamizi juu yenu, wakati baba zenu waliponikasirisha na sikuonyesha huruma,” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote, “hivyo sasa nimeazimia kufanya mema tena kwa Yerusalemu na Yuda. Msiogope. Haya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia yote haya,” asema BWANA.