Zekaria 7:11-14
Zekaria 7:11-14 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini watu walikataa kunisikiliza, wakakaidi na kuziba masikio yao ili wasisikie. Wakaifanya mioyo yao kuwa migumu kama jiwe, wasije wakasikia sheria yangu mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi niliyoitangaza kwa roho yangu kwa kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nikawaka hasira dhidi yao, nikasema, ‘Kwa kuwa niliwaita nao hawakunisikiliza, basi, nao waliponiita, sikuwasikiliza. Nami niliwatawanya kwa kimbunga kati ya mataifa yote ambayo hawakuyajua. Hivyo nchi waliyoiacha ikabaki tupu; hapakuwa na mtu yeyote aliyekaa humo; naam, nchi hiyo ya kupendeza ikawa ukiwa.’”
Zekaria 7:11-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini hao walikataa kusikiliza, wakageuza bega lao, wakaziba masikio yao ili wasisikie. Naam, walifanya mioyo yao kuwa kama jiwe gumu, wasije wakaisikia sheria na maneno ya BWANA wa majeshi, aliyoyatuma kwa roho yake, kwa mkono wa manabii wa kwanza; kwa sababu hiyo ghadhabu kuu ikatoka kwa BWANA wa majeshi. Ikawa kama wakati nilipowaita, wasitake kunisikiliza; basi, nao wataniita, wala sitasikiliza, asema BWANA wa majeshi. Lakini nitawatawanya kwa kimbunga kikali katikati ya mataifa yote wasiyoyajua. Basi nchi walioacha ikawa ya ukiwa, hata hapakuwa na mtu aliyeipitia akienda wala akirudi; maana waliifanya nchi iliyopendeza kuwa ukiwa.
Zekaria 7:11-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini hao walikataa kusikiliza, wakageuza bega lao, wakaziba masikio yao ili wasisikie. Naam, walifanya mioyo yao kuwa kama jiwe gumu, wasije wakaisikia sheria na maneno ya BWANA wa majeshi, aliyoyapeleka kwa roho yake kwa mkono wa manabii wa kwanza; kwa sababu hiyo ghadhabu kuu ikatoka kwa BWANA wa majeshi. Ikawa kwa sababu alilia, wao wasitake kusikiliza; basi, wao nao watalia, wala mimi sitasikiliza, asema BWANA wa majeshi. Lakini nitawatawanya kwa upepo wa kisulisuli, katikati ya mataifa yote wasiowajua. Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa ukiwa nchi baada yao, hata hapakuwa na mtu aliyepita kati yake, wala aliyerudi; maana waliifanya nchi iliyopendeza sana kuwa ukiwa.
Zekaria 7:11-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao. Wakaifanya mioyo yao migumu kama jiwe gumu na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo BWANA Mwenye Nguvu Zote aliyatuma kwa njia ya Roho wake kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo BWANA Mwenye Nguvu Zote alikasirika sana. “ ‘Wakati nilipoita, hawakusikiliza, kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. ‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”