Zekaria 6:9-15
Zekaria 6:9-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Pokea zawadi za watu walio uhamishoni zilizoletwa na Heldai, Tobia na Yedaya. Nenda leo hii nyumbani kwa Yosia, mwana wa Sefania ambamo watu hao wamekwenda baada ya kuwasili kutoka Babuloni. Utachukua fedha na dhahabu hiyo, utengeneze taji ambalo utamvika kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki, na kumwambia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Hapa pana mtu aitwaye Tawi. Yeye atastawi hapo alipo na kulijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu. Yeye ndiye atakayelijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu Atapewa heshima ya kifalme na kuketi kwenye kiti chake cha enzi kuwatawala watu wake. Karibu na kiti cha enzi cha mtawala huyo, atakaa kuhani mkuu, nao wawili watafanya kazi pamoja kwa amani. Taji hilo itahifadhiwa katika hekalu langu kwa heshima ya Heldai, Tobia, Yedaya na Yosia mwana wa Sefania.’ “Watu wanaokaa nchi za mbali watakuja kusaidia kulijenga hekalu langu mimi Mwenyezi-Mungu.” Nanyi mtajua kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndiye aliyenituma kwenu. Haya yote yatatukia kama mkiitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Zekaria 6:9-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo nenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli; naam, pokea fedha na dhahabu, ukatengeneze taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu; ukamwambie, ukisema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la BWANA. Naam, yeye atalijenga hekalu la BWANA; naye atakuwa na heshima ya kifalme; na ataketi na kutawala; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na maelewano yenye amani yatakuwa kati ya hao wawili. Na hayo mataji yatakuwa ya Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; yawe kumbukumbu katika hekalu la BWANA. Nao walio mbali watakuja na kusaidia kujenga hekalu la BWANA, nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu.
Zekaria 6:9-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA likanijia, kusema, Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo enenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli; naam, pokea fedha na dhahabu, ukafanye taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu; ukamwambie, ukisema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la BWANA. Naam, yeye atalijenga hekalu la BWANA; naye atauchukua huo utukufu; ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili. Na hizo taji zitakuwa za Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; ziwe ukumbusho katika hekalu la BWANA. Nao walio mbali watakuja na kujenga katika hekalu la BWANA, nanyi mtajua ya kuwa BWANA wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya BWANA, Mungu wenu.
Zekaria 6:9-15 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku hiyo hiyo nenda nyumbani mwa Yosia mwana wa Sefania. Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uliweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki. Umwambie hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Huyu ndiye mtu anayeitwa Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu. Ni yeye atakayejenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki kwenye kiti cha enzi. Atakuwa kuhani kwenye kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa na amani kati ya hao wawili.’ Taji litatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, nanyi mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa bidii.”