Zekaria 6:1-8
Zekaria 6:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba. Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi; na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu. Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu? Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote. Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wakatoka wakafuata nyuma yao; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hata nchi ya kusini. Na wale wekundu wakatoka, wakataka kwenda huko na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huko na huko katika dunia. Basi wakaenda huko na huko katika dunia. Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini.
Zekaria 6:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Niliona maono mengine tena. Safari hii, niliona magari manne ya farasi yakitoka katikati ya milima miwili ya shaba nyeusi. Gari la kwanza lilikokotwa na farasi wekundu, la pili lilikokotwa na farasi weusi, la tatu lilikokotwa na farasi weupe, na la nne lilikokotwa na farasi wa kijivujivu. Basi, nikamwuliza yule malaika aliyeongea nami, “Bwana, magari haya ya farasi yanamaanisha nini?” Malaika akanijibu, “Magari haya ni pepo kutoka pande nne za mbingu. Yalikuwa mbele ya Mwenyezi-Mungu wa dunia nzima, na sasa yanaondoka. Lile gari linalokokotwa na farasi weusi linakwenda kaskazini, lile linalokokotwa na farasi weupe linakwenda magharibi, na lile linalokokotwa na farasi wa kijivujivu linakwenda kusini.” Farasi hao walipotokea walikuwa na hamu sana ya kwenda kuikagua dunia. Naye malaika akawaambia, “Haya! Nendeni mkaikague dunia.” Basi, wakaenda na kuikagua dunia. Kisha yule malaika aliyeongea nami akaniambia kwa sauti, “Tazama! Wale farasi waliokwenda nchi ya kaskazini wameituliza ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.”
Zekaria 6:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba. Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi; na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu. Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu? Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote. Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wanatoka kwenda katika nchi ya magharibi; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hadi nchi ya kusini. Farasi wale walipotoka, walitaka kwenda huku na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huku na huko katika dunia. Basi wakaenda huku na huko katika dunia. Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini.
Zekaria 6:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba! Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi, la tatu lilivutwa na farasi weupe na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu. Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani bwana wangu?” Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake. Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.” Wakati hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote. Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaokwenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho yangu katika nchi ya kaskazini.”