Zekaria 14:16-21
Zekaria 14:16-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda. Iwapo taifa lolote duniani halitakwenda Yerusalemu kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, basi, mvua haitanyesha katika nchi yao. Iwapo Wamisri watakataa kuiadhimisha sikukuu ya vibanda, basi, Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa ugonjwa uleule atakaowapiga nao mataifa yote yanayokataa kuiadhimisha sikukuu hiyo. Hiyo itakuwa ndiyo adhabu itakayolipata taifa la Misri pamoja na mataifa yote yasiyoadhimisha sikukuu ya vibanda. Wakati huo, kwenye njuga za farasi yataandikwa maandishi haya: “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu Vyungu vilivyomo katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. Kila chungu katika mji wa Yerusalemu na nchi ya Yuda kitawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili wote wanaotoa tambiko waweze kuvichukua na kuchemshia nyama ya tambiko. Wakati huo, hakutakuwapo mfanya biashara yeyote katika hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Zekaria 14:16-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, na kuiadhimisha sikukuu ya Vibanda. Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, mvua haitanyesha kwao. Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo BWANA atawapiga mataifa, wasiokwea ili kuadhimisha sikukuu ya Vibanda. Hii ndiyo adhabu ya Misri, na adhabu ya mataifa yote, wasiokwea ili kuadhimisha sikukuu ya Vibanda. Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA BWANA; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya BWANA vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa BWANA wa majeshi; nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake; wala siku hiyo hatakuwamo tena mfanya biashara ndani ya nyumba ya BWANA wa majeshi.
Zekaria 14:16-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, na kuishika sikukuu ya Vibanda. Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, BWANA wa majeshi, mvua haitanyesha kwao. Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo BWANA atawapiga mataifa, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda. Hii ndiyo adhabu ya Misri, na adhabu ya mataifa yote, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda. Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA BWANA; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya BWANA vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa BWANA wa majeshi; nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake; wala siku hiyo hatakuwamo tena mfanya biashara ndani ya nyumba ya BWANA wa majeshi.
Zekaria 14:16-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha walionusurika katika mataifa yote ambayo yaliushambulia Yerusalemu watakuwa wakipanda Yerusalemu kila mwaka kumwabudu Mfalme, BWANA Mwenye Nguvu Zote na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. Ikiwa taifa lolote la dunia hawatakwenda Yerusalemu kumwabudu Mfalme, BWANA Mwenye Nguvu Zote, mvua haitanyesha kwao. Ikiwa watu wa Misri nao hawatakwenda kushiriki, hawatapata mvua. BWANA ataleta juu yao tauni ile ambayo itawapiga mataifa yale ambayo hayatakwenda kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. Hii itakuwa adhabu ya Misri na adhabu ya mataifa yote yale ambayo hayatakwenda Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. Katika siku hiyo, kengele zilizofungwa kwenye farasi zitaandikwa maneno haya: TAKATIFU KWA BWANA, navyo vyungu vya kupikia katika nyumba ya BWANA vitakuwa kama bakuli takatifu mbele ya madhabahu. Kila chungu kilichoko Yerusalemu na Yuda kitakuwa kitakatifu kwa BWANA Mwenye Nguvu Zote na wote wanaokuja kutoa dhabihu watachukua baadhi ya vyungu hivyo na kupikia. Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya BWANA Mwenye Nguvu Zote.