Zekaria 12:1-7
Zekaria 12:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ufunuo wa neno la BWANA juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo BWANA, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake. Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbayumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu. Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata majeraha mengi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake. Katika siku hiyo, asema BWANA, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hayo makabila ya watu. Na wakuu wa Yuda watasema mioyoni mwao, Wenyeji wa Yerusalemu wana nguvu katika BWANA wa majeshi, Mungu wao. Siku hiyo nitawafanya wakuu wa Yuda kuwa kama kigae chenye moto katika kuni, na kama kinga cha moto katika miganda; nao watateketeza watu wa kila kabila, wawazungukao pande zote, upande wa mkono wa kulia na upande wa mkono wa kushoto; na baada ya haya Yerusalemu utakaa mahali pake, naam, hapo Yerusalemu. Naye BWANA ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili utukufu wa nyumba ya Daudi, na utukufu wa wenyeji wa Yerusalemu, usipate kutukuzwa kuliko Yuda.
Zekaria 12:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ufunuo wa neno la BWANA juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo BWANA, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake. Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu. Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake. Katika siku hiyo, asema BWANA, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hizo kabila za watu. Na wakuu wa Yuda watasema mioyoni mwao, Wenyeji wa Yerusalemu ni nguvu zangu katika BWANA wa majeshi, Mungu wao. Siku hiyo nitawafanya wakuu wa Yuda kuwa kama kigae chenye moto katika kuni, na kama kinga cha moto katika miganda; nao watateketeza watu wa kila kabila, wawazungukao pande zote, upande wa mkono wa kuume na upande wa mkono wa kushoto; na baada ya haya Yerusalemu utakaa mahali pake, naam, hapo Yerusalemu. Naye BWANA ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili utukufu wa nyumba ya Daudi, na utukufu wa wenyeji wa Yerusalemu, usipate kutukuzwa kuliko Yuda.
Zekaria 12:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu kuhusu Israeli. Mwenyezi-Mungu aliyezitandaza mbingu, aliyeiweka misingi ya dunia na kumpa mwanadamu uhai asema hivi: “Nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama kikombe cha divai; na mataifa yaliyo kandokando yake yatakunywa na kuyumbayumba kama walevi. Mji wa Yerusalemu utakaposhambuliwa, hata miji yote ya Yuda itashambuliwa. Siku hiyo nitaufanya mji wa Yerusalemu kuwa kama jiwe zito kwa watu wote: Yeyote atakayelinyanyua atajiumiza mwenyewe. Watu wa mataifa yote duniani wataushambulia mji huo. Siku hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitamtia hofu kila farasi, na mpandafarasi wake nitamfanya kuwa mwendawazimu. Farasi wa mataifa mengine nitawapofusha. Lakini kabila la Yuda nitalilinda. Ndipo viongozi wa Yuda watakapoambiana, ‘Wakazi wa Yerusalemu wamepata nguvu yao kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao’. “Siku hiyo, viongozi wa Yuda nitawafanya kama chungu cha moto mkali katika msitu; naam, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watayateketeza mataifa yote yaliyo kandokando yao. Lakini watu wa Yerusalemu wataendelea kuishi salama katika mji wao. “Nami Mwenyezi-Mungu nitawasaidia kwanza jamaa za Yuda kusudi wazawa wa Daudi na wakazi wa Yerusalemu wasijione kuwa maarufu zaidi ya watu wengine wa kabila la Yuda.
Zekaria 12:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ni neno la BWANA kuhusu Israeli. BWANA, yeye azitandaye mbingu, awekaye misingi ya dunia na aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake, asema: “Nitakwenda kufanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbisha mataifa yote yanayoizunguka. Yuda utazingirwa kwa vita na Yerusalemu pia. Katika siku hiyo, wakati mataifa yote ya dunia yatakapokusanyika dhidi yake, nitaufanya Yerusalemu kuwa jabali lisilosogezwa kwa mataifa yote. Wote watakaojaribu kulisogeza watajiumiza wenyewe. Katika siku hiyo nitampiga kila farasi kwa hofu ya ghafula, naye ampandaye nitampiga kwa uwazimu,” asema BWANA. “Nitalielekeza jicho langu la ulinzi juu ya nyumba ya Yuda, nami nitawapofusha farasi wote wa mataifa. Kisha viongozi wa Yuda watasema mioyoni mwao, ‘Watu wa Yerusalemu wana nguvu kwa sababu BWANA Mwenye Nguvu Zote ni Mungu wao.’ “Katika siku hiyo nitawafanya viongozi wa Yuda kuwa kama kigae cha moto ndani ya lundo la kuni, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watateketeza kulia na kushoto mataifa yote yanayowazunguka, lakini Yerusalemu utabaki salama mahali pake. “BWANA atayaokoa makao ya Yuda kwanza, ili heshima ya nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu isiwe kubwa zaidi kuliko ile ya Yuda.