Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 4:1-22

Ruthu 4:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)

Boazi alikwenda mahali pa kufanyia mkutano huko kwenye lango la mji akaketi chini. Kisha yule ndugu ya Elimeleki ambaye Boazi alikuwa amemtaja, akapita karibu na hapo. Boazi akamwita, akasema, “Njoo, uketi hapa ndugu.” Basi huyo mtu akaja na kuketi hapo. Ndipo Boazi akawaita wazee kumi wa mji, akawaomba wao pia waketi hapo. Wakaketi. Ndipo Boazi akamwambia yule ndugu yake, “Sasa Naomi ambaye amerudi kutoka Moabu, anataka kuliuza shamba ambalo lilikuwa la jamaa yetu Elimeleki. Basi mimi nimeona afadhali nikujulishe habari hii. Sasa ikiwa unalitaka shamba hili, toa fidia ulichukue mbele ya wazee wa watu wangu. Ikiwa unalitaka au hulitaki sema basi kwa kuwa nafasi ya kwanza ya kulifidia ni yako na yangu ni ya pili.” Naye akasema, “Mimi nitalifidia.” Boazi akasema, “Ni vyema, lakini ukilichukua hilo shamba kutoka kwa Naomi, basi utakuwa unamchukua pia Ruthu Mmoabu, mjane ambaye ni jamaa ya marehemu ili kwamba shamba hilo libaki katika jamaa ya huyo marehemu.” Yule jamaa aliyekuwa wa karibu akajibu, “Ikiwa ni hivyo, sitalifidia shamba hilo, kwa sababu yaonekana kuwa nitauharibu urithi wangu. Afadhali haki yangu ya kulichukua nikupe wewe, maana mimi siwezi kulifidia.” Siku zile, katika Israeli ikiwa watu walitaka kukomboa au kubadilishana kitu, ilikuwa ni desturi kwa mtu kuonesha ishara kwa kuvua kiatu chake na kumpa mwingine. Kwa ishara hiyo Waisraeli walionesha kwamba mambo yamesawazishwa. Basi, mtu huyo alimwambia Boazi, “Lifidie shamba,” kisha alivua kiatu chake na kumpa. Ndipo Boazi akawaambia wazee na watu waliokuwa hapo, “Leo nyinyi ni mashahidi wangu. Mmeona kwamba nimenunua kutoka kwa Naomi, vyote vilivyokuwa vya Elimeleki, na vya Kilioni na Mahloni. Zaidi ya hayo, Ruthu Mmoabu mjane wa Mahloni, nimemnunua ili awe mke wangu. Mapatano haya yatafanya mali ya jamaa ya marehemu na ukoo wake kubakia kwa watu wake katika mji huu. Nyinyi ni mashahidi.” Basi wazee waliokuwa langoni na watu wote waliokuwapo walijibu, “Ndiyo, sisi ni mashahidi. Mwenyezi-Mungu amfanye mke wako awe kama Raheli na Lea, ambao wote wawili waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe upate kustawi katika jamaa ya Efratha, uwe na sifa katika Bethlehemu. Kwa sababu ya watoto Mwenyezi-Mungu atakaokupatia ambao mwanamke huyu atakuzalia, nayo nyumba yako iwe kama nyumba ya Peresi ambaye Tamari alimzalia Yuda.” Kwa hiyo, Boazi akamchukua Ruthu akawa mke wake. Mwenyezi-Mungu alimjalia Ruthu naye akachukua mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Ndipo wanawake wa mji huo wakamwambia Naomi, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye hakukuacha leo bila kuwa na jamaa aliye karibu wa kukutunza; naye awe mwenye sifa kubwa katika Israeli. Yeye atakurudishia uhai wako na atakutunza katika uzee wako; maana mkwe wako anayekupenda ambaye ana thamani kubwa zaidi kwako kuliko watoto wa kiume saba, ndiye amemzaa.” Basi Naomi alimchukua mtoto huyo akamweka kifuani mwake na kumlea. Wanawake majirani walimwita mtoto huyo Obedi wakisema, “Mtoto amezaliwa kwa Naomi.” Hatimaye Obedi akamzaa Yese aliyemzaa Daudi. Na hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Rami, Rami akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nahshoni, Nahshoni akamzaa Salmoni, Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi, Obedi akamzaa Yese na Yese akamzaa Daudi.

Shirikisha
Soma Ruthu 4

Ruthu 4:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi. Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi. Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki; nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi. Ndipo Boazi aliposema, Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu, ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake. Basi yule jamaa aliyekuwa wa karibu akasema, Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafsi yangu, nisije nikauharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa. Basi hii ilikuwa desturi zamani za kale katika Israeli, kwa habari ya kukomboa na kubadilishana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israeli. Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake. Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi. Tena, huyu Ruthu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi. Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. BWANA na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu. Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa BWANA katika mwanamke huyu. Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na BWANA akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume. Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe BWANA, asiyekuacha leo ukiwa huna jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli. Naye atakurejeshea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto saba, ndiye aliyemzaa. Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake. Nao wale wanawake waliokuwa jirani zake wakampa jina, wakisema, Naomi amezaliwa mwana; wakamwita jina lake Obedi; yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi. Hivi ndivyo vizazi vya Peresi; Peresi alimzaa Hesroni; na Hesroni akamzaa Ramu; na Ramu akamzaa Aminadabu; na Aminadabu akamzaa Nashoni; na Nashoni akamzaa Salmoni; na Salmoni akamzaa Boazi; na Boazi akamzaa Obedi; na Obedi akamzaa Yese; na Yese akamzaa Daudi.

Shirikisha
Soma Ruthu 4

Ruthu 4:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi. Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi. Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki; nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi. Ndipo Boazi aliposema, Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu, ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake. Basi yule jamaa aliyekuwa wa karibu akasema, Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafsi yangu, nisije nikauharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa. Basi hii ilikuwa desturi zamani za kale katika Israeli, kwa habari ya kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israeli. Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake. Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi. Tena, huyu Ruthu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi. Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. BWANA na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu. Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa BWANA katika mwanamke huyu. Basi Boazi akamtwaa Ruthu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na BWANA akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume. Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe BWANA, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli. Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto saba, ndiye aliyemzaa. Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake. Nao wale wanawake waliokuwa jirani zake wakampa jina, wakisema, Naomi amezaliwa mwana; wakamwita jina lake Obedi; yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi. Hivi ndivyo vizazi vya Peresi; Peresi alimzaa Hesroni; na Hesroni akamzaa Ramu; na Ramu akamzaa Aminadabu; na Aminadabu akamzaa Nashoni; na Nashoni akamzaa Salmoni; na Salmoni akamzaa Boazi; na Boazi akamzaa Obedi; na Obedi akamzaa Yese; na Yese akamzaa Daudi.

Shirikisha
Soma Ruthu 4

Ruthu 4:1-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Boazi akakwea mpaka kwenye lango la mji, akaketi pale. Yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa, rafiki yangu. Karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi. Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi. Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki. Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.” Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.” Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.” Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.” (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.) Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake. Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni. Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!” Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. BWANA na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrathi na uwe mashuhuri katika Bethlehemu. Kupitia kwa watoto ambao BWANA atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.” Basi Boazi akamwoa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, BWANA akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume. Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe BWANA, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote! Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.” Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake. Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina lake Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi. Hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Ramu, Ramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni, Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi, Obedi akamzaa Yese, na Yese akamzaa Daudi.

Shirikisha
Soma Ruthu 4

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha