Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 1:1-18

Ruthu 1:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Wakati Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi. Mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda, pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu. Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu, wakaishi huko. Elimeleki mumewe Naomi akafa, hivyo Naomi akabaki na wanawe wawili. Nao wakaoa wanawake Wamoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya kama miaka kumi, Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili. Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba BWANA amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakweze wakajiandaa kurudi nyumbani. Yeye na wakweze wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda. Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe zake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani kwa mama yake. BWANA na awatendee fadhili kama mlivyowatendea hao waliofariki, na pia mimi. BWANA na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani kwa mume mwingine.” Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa, wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe nyumbani kwa watu wako.” Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi? Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana, je, mngesubiri mpaka wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa BWANA umekuwa kinyume nami!” Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye. Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.” Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. BWANA na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.

Shirikisha
Soma Ruthu 1

Ruthu 1:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo zamani, wakati waamuzi walipokuwa wanatawala Israeli, palitokea njaa nchini humo. Mtu mmoja kutoka Bethlehemu katika Yuda pamoja na mkewe na watoto wao wa kiume wawili walikwenda kuishi kwa muda nchini Moabu ili kuishi kama wageni. Mtu huyo aliitwa Elimeleki na mkewe aliitwa Naomi. Watoto wao wawili wa kiume, mmoja aliitwa Mahloni na mwingine Kilioni. Mtu huyo na jamaa yake walikuwa Waefrathi wa huko Bethlehemu katika Yuda. Walikwenda nchini Moabu, wakakaa huko. Lakini Elimeleki, mumewe Naomi, alifariki na Naomi akaachwa na wanawe wawili. Vijana hao walioa wasichana wa Kimoabu, Orpa na Ruthu. Baada ya miaka kumi hivi, Mahloni na Kilioni nao pia walifariki. Baadaye, Naomi alipata habari kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa amewabariki watu wake kwa kuwapa chakula. Basi, akaondoka kutoka Moabu kurudi kwao pamoja na wakwe zake. Akaondoka mahali pale alipoishi pamoja na wakwe zake, wakashika njia ya kurudi Yuda. Naye Naomi akawaambia hao wakwe zake wawili, “Rudini kila mmoja nyumbani kwa mama yake. Naomba Mwenyezi-Mungu awe mwema kwenu kama mlivyokuwa wema kwangu na kwa wale watu wangu waliofariki. Mwenyezi-Mungu awajalie, kila mmoja wenu apate mume na nyumba yake.” Kisha Naomi akawaaga kwa kuwabusu. Lakini wao walianza kulia kwa sauti na kumwambia, “La hasha! Tutakwenda pamoja nawe kwa watu wako.” Naye Naomi akawasihi, “Rudini, binti zangu. Kwa nini kunifuata? Je, mnafikiri naweza kupata tena watoto watakaokuwa waume zenu? Rudini nyumbani kwenu binti zangu, kwa maana mimi ni mzee mno, siwezi kuolewa tena. Hata kama ningesema ninalo tumaini, na hata kama ningepata mume usiku huu na kupata watoto, je, mngeweza kungoja mpaka wakue? Je, mngeweza kujizuia msiolewe na waume wengine? Sivyo, binti zangu! Mambo yangu ni magumu mno kwa ajili yenu, maana Mwenyezi-Mungu amenipiga kipigo.” Hapo walipaza sauti wakaanza kulia tena. Ndipo Orpa akamkumbatia mkwewe, akamuaga na kurudi nyumbani; lakini Ruthu, akaandamana naye. Basi Naomi akamwambia, “Ruthu, tazama dada yako amerudi nyumbani kwake na kwa mungu wake; basi, nawe pia urudi, umfuate dada yako.” Lakini Ruthu akamjibu, “Usinisihi nikuache wewe, wala usinizuie kufuatana nawe. Kokote utakakokwenda ndiko nami nitakakokwenda, na ukaapo nitakaa, watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. Pale utakapofia hapo nitakufa nami, na papo hapo nitazikwa; Mwenyezi-Mungu anipe adhabu kali kama nikitenganishwa nawe isipokuwa tu kwa kifo.” Naomi alipoona kuwa Ruthu ameamua kwenda pamoja naye, aliacha kumshawishi.

Shirikisha
Soma Ruthu 1

Ruthu 1:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hapo zamani Waamuzi walipokuwa wanatawala, njaa ilitokea katika nchi. Mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaondoka akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrata wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko. Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Baada ya kukakaa huko miaka kumi hivi, wote wawili Maloni na Kilioni wakafa; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana akiwa katika nchi ya Moabu alipata habari kuwa BWANA alikuwa amewajia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwa akiishi, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, rudini; kwa nini mfuatane nami? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, dada yako amerudi kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urudi nawe ukamfuate dada yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirudi nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapofia ndipo nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo hivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekata shauri kufuatana naye, aliacha kumshawishi.

Shirikisha
Soma Ruthu 1

Ruthu 1:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa zamani za Waamuzi walipoamua, kulikuwa na njaa katika nchi. Akaondoka mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrathi wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko. Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba BWANA amewajilia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye.

Shirikisha
Soma Ruthu 1