Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 8:1-39

Waroma 8:1-39 Biblia Habari Njema (BHN)

Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu wa binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi. Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani. Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmefanywa kuwa waadilifu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu. Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi. Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!” Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake. Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu. Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu. Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake. Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka kwa wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 8

Waroma 8:1-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho. Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina uchungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa tumaini; lakini kitu kilichotumainiwa kikionekana, hakiwi tumaini tena. Kwa maana ni nani anayekitumainia kile akionacho? Bali tukikitumainia kitu tusichokiona, twakingojea kwa subira. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza. Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani awezaye kutupinga? Yeye ambaye hakumhurumia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje pia kutupa chochote kingine pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kulia wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote sisi ni zaidi ya washindi, kupitia kwake yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 8

Waroma 8:1-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho. Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye. Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza. Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 8

Waroma 8:1-39 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo. Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki. Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu. Kwa hiyo ndugu zangu, sisi tu wadeni, si wa mwili, ili tuishi kwa kuufuata mwili, kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye. Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu. Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari? Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi. Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu. Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale Mungu aliowajua tangu mwanzo, pia aliwachagua tangu mwanzo, wapate kufanana na mfano wa Mwanawe, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Nao wale Mungu aliotangulia kuwachagua, akawaita, wale aliowaita pia akawahesabia haki, nao wale aliowahesabia haki, pia akawatukuza. Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye? Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? Kama ilivyoandikwa: “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 8

Waroma 8:1-39

Waroma 8:1-39 BHNWaroma 8:1-39 BHNWaroma 8:1-39 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha