Waroma 7:7-13
Waroma 7:7-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, tuseme basi, kwamba sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama sheria isingalikuwa imesema: “Usitamani.” Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila sheria dhambi ni kitu kilichokufa. Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka, nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo. Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua. Basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri. Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Ilivyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno.
Waroma 7:7-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? La hasha! Lakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani. Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa. Nami nilikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa. Nikaona ya kuwa ile amri iletayo uzima kwangu mimi ilileta mauti. Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua. Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? La hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa, ilifanya mauti ndani yangu kwa njia ya ile njema, kusudi kwa ile amri dhambi izidi kuwa mbaya mno.
Waroma 7:7-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani. Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa. Nami nalikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa. Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti. Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua. Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? Hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa, ilifanya mauti ndani yangu kwa njia ya ile njema, kusudi kwa ile amri dhambi izidi kuwa mbaya mno.
Waroma 7:7-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini, isingekuwa kwa sababu ya sheria, nisingalijua dhambi. Nisingalijua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.” Lakini dhambi kwa kupata nafasi katika amri, hii ikazaa ndani yangu kila aina ya tamaa. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa. Wakati fulani nilikuwa hai pasipo sheria, lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa. Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti. Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua. Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema. Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kwa njia ya amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi.