Waroma 7:15-25
Waroma 7:15-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachokichukia ndicho nikifanyacho. Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile sheria ni nzuri. Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi inayokaa ndani yangu. Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza. Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka. Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. Basi, nimegundua kanuni hii: Ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua. Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu. Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu. Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka mwili huu unaonipeleka kifoni? Shukrani kwa Mungu afanyaye hivyo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo! Hii basi, ndiyo hali yangu: Mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya Mungu, lakini kwa mwili wangu ninaitumikia sheria ya dhambi.
Waroma 7:15-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema siwezi. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka wa ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.
Waroma 7:15-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.
Waroma 7:15-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote likaalo ndani yangu, yaani, katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu. Ole wangu mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Ashukuriwe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.