Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 5:1-21

Waroma 5:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu. Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia. Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia, alikufa kwa ajili yetu sisi waovu. Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. Kwa kuwa sasa tumefanywa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu. Maana, tulipokuwa bado maadui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uhai wa Kristo. Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu. Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi. Kabla ya sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria. Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu. Adamu alikuwa kielelezo cha Kristo ambaye alikuja baadaye. Lakini kosa la Adamu haliwezi kulinganishwa na neema ya Mungu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake. Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe. Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja, kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kufanywa kuwa waadilifu, watatawala katika uhai kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo. Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kiadilifu cha mtu mmoja kinawapa wote uadilifu na uhai. Na kama kwa kutokutii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi kuwa waadilifu. Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi. Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa uadilifu na kuleta uhai wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 5

Waroma 5:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na muwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta subira; na kazi ya subira ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho. Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; lakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 5

Waroma 5:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho. Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi. Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo. Basi tena, kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 5

Waroma 5:1-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia. Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho. Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi: kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria. Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Mose, mauti ilitawala watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama alivyofanya Adamu, ambaye alikuwa mfano wa yule atakayekuja. Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, zaidi sana neema ya Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi. Tena, ile karama ya Mungu si kama matokeo ya ile dhambi. Hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja, ikaleta adhabu, bali karama ya neema ya Mungu ilikuja kwa njia ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo. Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote. Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki. Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi, ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata kuleta uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.

Shirikisha
Soma Waroma 5