Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 4:1-25

Waroma 4:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu? Kama Abrahamu alikuwa amefanywa mwadilifu kutokana na bidii yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu. Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake. Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, akamkubali kuwa mwadilifu. Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu yule ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake: “Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa. Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.” Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa. Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu. Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu. Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna sheria, haiwezekani kuivunja. Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: Si kwa wale tu wanaoishika sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini-Mungu ambaye huwapa wafu uhai, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa. Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Wazawa wako watakuwa wengi kama nyota!” Alikuwa mzee wa karibu miaka 100, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa. Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu. Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi. Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu. Inaposemwa, “Alimkubali,” haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu. Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka kwa wafu. Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tufanywe waadilifu.

Shirikisha
Soma Waroma 4

Waroma 4:1-25 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo: “Wamebarikiwa wale ambao wamesamehewa makosa yao, ambao dhambi zao zimefunikwa. Heri mtu yule Bwana hamhesabii dhambi zake.” Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa. Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako. Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.” Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.” Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.

Shirikisha
Soma Waroma 4

Waroma 4:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi, tusemeje juu ya Abrahamu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. Maana Maandiko yasemaje? Abrahamu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. Kama vile Daudi ainenavyo heri yake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi. Basi je! Heri hiyo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa tunanena ya kwamba kwake Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, mhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Abrahamu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa. Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Abrahamu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika. Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazawa wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Abrahamu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia moja), na hali ya utasa wa tumbo lake Sara. Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutoamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki. Lakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

Shirikisha
Soma Waroma 4

Waroma 4:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo, Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi. Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa. Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika. Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara. Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki. Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake; bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

Shirikisha
Soma Waroma 4