Waroma 15:14-21
Waroma 15:14-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”
Waroma 15:14-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, mimi mwenyewe nina hakika juu yenu, kuwa ninyi mmejaa wema, na mmejazwa ujuzi wote, tena mnaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kandokando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiowahi kuhubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiowahi kusikia habari zake watafahamu.
Waroma 15:14-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu.
Waroma 15:14-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema, mkijazwa ufahamu wote na mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi. Hata hivyo, nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu ili kuwakumbusha tena kuvihusu, kutokana na ile neema Mungu aliyonipa niwe mhudumu wa Al-Masihi Isa kwa watu wa Mataifa. Alinipa huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubalika na Mungu, kwa kutakaswa na Roho wa Mungu. Kwa hiyo ninajisifu katika Al-Masihi Isa, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Al-Masihi amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake hadi Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Al-Masihi kwa ukamilifu. Hivyo imekuwa nia yangu kuhubiri Injili pale ambapo Al-Masihi hajajulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Lakini kama ilivyoandikwa: “Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona, nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”