Waroma 15:1-7
Waroma 15:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni.
Waroma 15:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe. Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe. Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Matusi yao waliokutusi wewe yalinipata mimi. Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini. Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunuia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe.
Waroma 15:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe. Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe. Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Malaumu yao waliokulaumu wewe yalinipata mimi. Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini. Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe.
Waroma 15:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini. Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.