Waroma 12:6-11
Waroma 12:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha. Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima. Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
Waroma 12:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa ni unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa ni huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; msimamizi, na asimamie kwa bidii; anayerehemu, na arehemu kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkilishika lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, bila kulegea; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana
Waroma 12:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana
Waroma 12:6-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha. Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana Isa.